• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2012

    NIYONZIMA AWAPA UBINGWA STARS

    Niyonzima kushoto akibadilishana bendera na nahodha wa Bara, Juma Kaseja Lugogo jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    NAHODHA wa Rwanda, Haruna Niyonzima amewatabiria Tanzania Bara kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu.
    Kiungo huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam aliyasema hayo baada ya mechi ya Robo Fainali jana Uwanja wa Lugogo baina ya nchi hizo mbili, ambayo Bara walishinda mabao 2-0.
    “Tumekubaliana na matokeo, sisi tulishindwa kutumia nafasi, wenzetu walicheza vizuri na walitumia nafasi, tunakubali huo ndio mpira sisi tumetolewa,”alisema.
    Niyonzima aliisifu Bara kucheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu na akasema kama wataendelea hivyo, basi watarejea na Kombe Dar es Salaam. “Kila mtu alikuwa anatekeleza majukumu yake vizuri uwanjani na kwa kweli mimi nawapongeza,”alisema.
    Bara ilifanikiwa kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa.
    Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
    Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
    Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.
    Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.
    Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
    Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NIYONZIMA AWAPA UBINGWA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top