• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2012

    SIMBA NA YANGA KAMA MNA JEURI ILETENI KWA KIFAA HIKI

    David Obua kushoto na BIN ZUBEIRY Lugogo, Kampala jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    SIMBA SC, Azam na Yanga, kama wana jeuri wailete hapa Kampala, Uganda kugombea saini ya mchezaji aliyekuwa anakipiga Ulaya.
    Huyo si mwingine zaidi ya kiungo wa kimataifa wa Uganda, David Obua ambaye amemaliza mkataba wake katika klabu ya Hearts ya Ligi Kuu ya Scotland na hataki kuongeza, ingawa pia amekuwa mgumu kuelezea mikakati yake mipya.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Obua alisema kwamba amemaliza mkataba wake Hearts na kwa sasa yupo tu nyumbani Kampala. Alipoulizwa kuhusu mikakati yake mipya, Obua alisema; “Sina cha kusema,”.
    David amekuwa akifuatilia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini hapa tangu yameanza Novemba 24 na jana alikuwapo Uwanja wa Lugogo kushuhudia Zanzibar na Bara zinazotengeneza Muungano wa Tanzania zikitinga Nusu Fainali.
    David ni mtoto marehemu Denis Obua, ambaye aliichezea Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na ana mdogo wake, Eric Obua ambaye pia anachezea The Cranes.
    Mjomba wake, John Akii-Bua aliweka rekodi ya kuwa bingwa wa kwanza Mganda wa Olimpiki kwa kushinda mita 400 huku akiweka rekodi ya dunia ya kutumia muda wa dakika 47 na sekunde 82 mwaka 1972  mjini Munich, Ujerumani.
    David Obua, alizaliwa Aprili 10 mwaka 1984 mjini Kampala, Uganda na kisoka aliibukia katika klabu ya Polisi mwaka 1999, kabla ya mwaka 2001 kusajiliwa Express ‘Red Eagles’ alikocheza hadi mwaka 2002      alipohamia AS Port-Louis ya Mauritius ambako alicheza msimu mmoja na kurejea Express alikocheza hadi 2005 alipohamia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
    Lakini pia, David wakati anasoma Marekani, alizichezea kwa muda klabu za Raleigh na Wilmington Hammerheads za nchini humo.
    Mwaka 2008, David alitua Ulaya katika klabu ya Hearts ambako hadi anamaliza mkataba wake amecheza jumla ya mechi 91 na kuifungia mabao sita.
    Tangu mwaka 2003, Obua amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda    na katika kipindi chote hicho, ameichezea Cranes mechi 27 na kuifungia mabao 14.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA KAMA MNA JEURI ILETENI KWA KIFAA HIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top