• HABARI MPYA

    Tuesday, December 11, 2012

    SIMBA SC WAENDA UARABUNI KUSAKA MAKALI

    Kikosi cha Simba kilichocheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara

    Na Mahmoud Zubeiry
    MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kwenda Oman kuweka kambi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Habari kutoka ndani ya Simba, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Simba itakwenda nchini humo kwa mwaliko wa klabu kongwe ya huko, Fanja FC.
    Ikiwa huko, Simba itacheza pia mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu tishio katika Ligi Kuu ya Oman, wakiwemo wenyeji wao hao, Fanja FC.
    Simba inakuwa timu ya tatu ya Ligi Kuu kuwa katika mpango wa ziara ya nje ya nchi, baada ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga na Azam nao kutangaza ziara zao.
    Wakati Azam watakwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndani ya siku mbili hizi, Yanga watakwenda Uturuki mwishoni mwa mwezi huu.
    Mbali na Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa, mapema Januari Simba na Yanga zitacheza pia Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo itafanyika mjini Kigali, Rwanda.
    Yanga watakwenda kama mabingwa watetezi, baada ya kutwaa Kombe hilo Julai mwaka huu mjini Dar es Salaam, wakati Simba watakwenda kwa tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo, wakiwa mabingwa wa Bara.
    Kwa miaka miwili mfululizo, timu za Bara zinaonekana kurejesha utawala wake kwenye michuano hiyo, kutokana na fainali mbili mfululizo zilizopita kuzikutanisha timu za Tanzania tupu.
    Mwaka 2011, Yanga iliifunga Simba SC 1-0, bao pekee la Mghana Kenneth Asamoah na kutwaa taji la nne, wakati mwaka huu Watoto hao wa Jangwani, walikutana na Azam FC katika mchezo wa Kombe uwanjani na kushinda 2-0, mabao ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi.
    Azam, Simba na Yanga kwa sasa ndio washindani wa taji la Ligi Kuu nchini, ambao wanaonekana kutaka kujiimarisha vizuri kabla ya kuanza kwa hatua ya lala salama ya ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC WAENDA UARABUNI KUSAKA MAKALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top