• HABARI MPYA

    Wednesday, December 12, 2012

    UGANDA ONE ANAMWAGA WINO LEO SIMBA SC

    Dhaira anajitia kitanzi leo Msimbazi

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIPA namba moja wa Uganda, Abbel Dhaira leo anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia Simba baada ya kutua jana jioni mjini Dar es Salaam akitokea kwao Uganda.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema kwamba, baada ya kusaini leo, Dhaira atarejea kwao mara moja kwa ajili ya kwenda kujiandaa kuja kuanza kazi rasmi Msimbazi.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliyepigana vita dhidi ya Uganda, alisema kwamba Dhaira hatachelewa kurejea kuanza kumtumikia mwajiri wake mpya, bali atakuja mapema.
    Dhaira amekwishasema atafurahi kujiunga na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na angependa kuungana na Mganda mwenzake, Emmanuel Okwi huko.
    Tayari Simba SC imefikia makubaliano na kipa huyo namba moja wa Uganda, aliyemaliza mkataba wake na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dau ambalo halijafahamika.
    Dhaira alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba kusaini mkataba wa miaka miwili kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
    Dhaira aliyeibukia Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
    Ikimpata Dhaira, Simba SC itakuwa imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
    Katika mechi za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
    Kwa sababu hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema hataki tena kuchezea Simba.
    Lakini pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UGANDA ONE ANAMWAGA WINO LEO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top