• HABARI MPYA

    Tuesday, May 08, 2012

    AZIM DEWJI KACHANGIA SANA KIPIGO CHA 5-0 YANGA


    SIRI ya mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi kujituma na kuwa nyota wa mchezo dhidi ya watani wa jadi, Simba SC ni ahadi nono aliyopewa na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Hussein Hasham Dewji (pichani kushoto), BIN ZUBEIRY imeipata hiyo.
    Habari kutoka ndani ya Simba SC, zimesema kwamba wakati timu hiyo inaingia kwenye mchezo dhidi ya watani hao wa jadi, Yanga- hofu yao ilikuwa juu ya Okwi mshambuliaji ambaye pamoja na makali yake, awali tangu ajiunge na timu hiyo miaka mitatu iliyopita, hakuwahi kutikisa nyavu za Yanga.
    Lakini mchezo wa Mei 6, 2012 kwa kujua kabisa yeye ni tegemeo la timu hiyo, aliwekewa mikakati mizito ili siku hiyo acheze soka yake yote na kuibeba timu.
    “Ilibidi Dewji, ambaye kwa kweli hivi sasa anaisaidia sana SImba ingawa tu hajitangazi, akae naye na kumpa ahadi nono, alimuambia kila bao analofunga anampa Milioni moja. Na kila pasi ya bao anampa 500,000.
    Sasa amekula fedha ya mabao mawili ya kufunga na zile penalti mbili alizosababisha inakuwa sawa na pasi za mabao. Na Dewji alimpa fedha zake zote siku ile ile baada ya mechi,”kilisema chanzo chetu kutoka Simba SC.
    Katika siku za karibuni, Dewji amekuwa akiisaidia mno Simba, na hiyo inatokana na umoja aliourejesha Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage kwenye klabu hiyo tangu aingie madarakani, kwani hata kundi la Friends Of Simba nalo linasaidia timu sasa.
    Dewji ni mfadhili wa kihistoria ndani ya SImba, ambaye ana mchango mkubwa mno kwenye mafanikio ya kihistoria ya klabu hiyo.
    Juhudi zake ndizo ziliipa SImba mataji manne ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame, katika miaka ya 1991, 1992, 1995 na 1996 na mwaka 1993 aliiwezesha klabu hiyo kufika fainali ya Kombe la CAF.
    Okwi
    Lakini kutokana na migogoro, mwaka 1996 Dewji alijitoa na SImba kuinunua iliyokuwa SIgara SC, ambayo hata hivyo ilishushwa Daraja la FAT kwa kosa la kumtumia kipa Manyika Peter bila kukamilisha taratibu za uhamisho wake kutoka Mtibwa Sugar.
    Baadaye Sigara ilinunuliwa na Mtanzania anayeishi Marekani, Alexander Otaqs Kajumulo na tangu hapo, Dewji alibaki kama mdau wa kawaida wa soka.
    Lakini katika kipindi chote hicho ameendelea kusaidia soka.
    Bado Dewji huwezi kumtenganisha na mafanikio ya timu ya taifa ya Bara kutwaa Kombe la Challenge mwaka 1994 nchini Kenya, kwani yeye ndiye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya timu.  
    Dewji ambaye amewekeza hadi nchini Zambia, timu ya taifa ya nchi hiyo< chipolopolo ilipotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika, mapema mwaka huu aliizawadia pia.
    Mwaka juzi, alikuwa miongoni mwa Wakurugenzi wa Moro United, ambayo hata hivyo baadaye alijitoa kutokana na kujitokeza watu wenye mlengo wa kushoto.
    Okwi akimburuza Nsajigwa
    Hivi karibuni, Dewji amemwaga mamilioni kibao kumsajili Simba kiungo baab kubwa, Nizar Khalfan aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Marekani, katika klabu ya Simba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZIM DEWJI KACHANGIA SANA KIPIGO CHA 5-0 YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top