SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema
limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji,
Amir Roshan (pichani kushoto) akiwa jijini Dar es Salaam.
Ofisa wa Habari wa TFF, Boniphace Wambura
amesema leo katika taarifa aliyotuma BIN ZUBEIRY kwamba Roshan alikuwa
akiwakilisha mikoa ya Kagera na Shinyanga na alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu
tangu afanyiwe operesheni ya kichwa mwishoni mwa mwaka 2010.
Roshan ambaye alianza kuingia kwenye
uongozi wa TFF wakati huo ikiwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika
uchaguzi uliofanyika mjini Kibaha mwaka 1993, amezikwa jana mchana kwenye
makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF kwa vipindi vitano mfululizo. Alichaguliwa katika uchaguzi wa
mwaka 1993, jijini Dar es Salaam (1996), jijini Arusha (2001), jijini Dar es
Salaam (2004) na jijini Dar es Salaam (2008).
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
ameelezea masikitiko yake na mshtuko mkubwa kutokana na kifo cha kiongozi huyo
wa muda mrefu kwenye mpira wa miguu, hasa Kanda ya Ziwa akiwa Mwenyekiti wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA).
Osiah amesema TFF inatoa pole kwa ndugu,
jamaa, marafiki na familia ya mpira wa miguu kwa kumpoteza ndugu yao kipenzi,
na Shirikisho litamkumbuka kwa mchango wake kwenye mpira wa miguu na dhamana
aliyoibeba kwa muda mrefu akiongoza mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa na
Taifa.
Msiba huu ni pigo kwa familia ya Roshan,
TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa
kwa Tanzania hasa akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji.
Mungu aiweke roho ya marehemu Amir Roshan
mahali pema peponi. Amina
0 comments:
Post a Comment