• HABARI MPYA

    Sunday, May 06, 2012

    KUBORONGA YANGA MSIMU HUU, WOTE WANAHUSIKA


    Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimkabidhi kombe nahodha wa timu ya Simba Juma K. Juma baada ya timu ya Simba kuifunga Yanga magoli 5-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar salaam katika mchezo uliokuwa ni wa  kumaliza michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom uliomalizika jioni hii  kwenye uwanja wa Taifa, huku ikiwa tayari ni mabingwa wapya wa ligi hiyo, Simba imefanikiwa kutunza heshima yake baada ya kuifunga Yanga magoli 5 kupitia wachezaji wake Emmanuel Okwi, goli la kwanza.  

    Goli la pili la Simba likafungwa na mchezaji Felix Sunzu kwa njia ya penati na dakika chache baadae Emmanuel Okwi akaongeza goli la tatu , Juma Kaseja akaongeza goli la nne kwa penati wakati pia Patrick Mafisango akafunga hesabu kwa kufunga  goli la tano baada ya wachezaji wa Yanga kufanya makosa katika eneo la hatari  

    Mchezaji wa timu ya Simba mganda Emmanuel Okwi akishangilia goli mara baada ya kuifungia timu yake goli la kuongoza
    Wachezaji wa Simba wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe  leo kwenye uwanja wa Taifa jioni hii.
    Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimvisha Medali mtoto wa mchezaji Uhuru Selemani wa Simba.
    Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimvisha medali mshabuliaji wa Simba Emmanuel Okwi.
    Wachezaji wa timu ya Simba wakishangilia na kocha wao kwa kumbeba juu juu.
    Luninga kubwa ya uwanjani ikionyesha magoli yaliyofungwa na Simba
    PICHA ZOTE KWA HISANI YA FULL SHANGWE....


    JIONI hii almanusra historia ijirudie Uwanja wa mpya wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga kufungwa 6-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
    Lakini ‘Mungu’ saidia bao la sita liligoma- liligoma kabisa, ingawa Yanga wenyewe, kama jogoo ambaye amekwishakanyagwa bawa na miguu, walikuwa wamekwishanyoosha shingo tayari kuchinjwa.
    Simba SC wamepokea Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa furaha isiyo na kifani, kwenye Uwanja wa Taifa, baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0.
    Mabao hayo yalifungwa na Emanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mafisango wote kwa penalti.
    Hii ni mara ya kwanza katika pambano la watani, timu moja kupewa penalti zaidi ya moja mchezoni na kipigo hiki hakika kimewanyong’onyesha kabisa mashabiki wa Yanga.
    Baadhi wamezimia uwanjani leo- na hapana shaka hadi kesho taarifa zaidi za kusikitisha zitaibuka.
    Wapo watakaoamini kipigo hiki kinatokana na mgogoro unaoendelea klabuni- lakini watasahau kuzungumzia sababu za kiufundi, hususan udhaifu wa timu.
    Nsajigwa leo peke yake unaweza kuendelea kuiota sura yake hata miaka 10 baadaye kila ukikumbuka kipigo cha leo, kama ambavyo zile 6-0 bado wana Yanga wanamkumbuka Bernad Madale.
    Mapema tu baada ya kukamilisha usajili wake, niliandika makala wakati huo bado nipo gazeti la DIMBA nikiwaambia Yanga, kuna mapungufu kwenye kikosi chao.
    Hawakusajili beki wa kati imara na kiungo wa ulinzi pia- zaidi walijaza mabeki kulia na kushoto. Yanga haina kiungo mkabaji na zaidi usajili uliofanyika ni kwa matakwa ya uongozi na hawakufuata ushauri wa kocha wao wakati huo, Sam Timbe, ambaye baadaye walimfukuza wakidai hashauriki.
    Walisajili kwa mazoea na historia badala ya kuangalia uwezo wa mchezaji katika wakati husika- matokeo yake msimu huu Yanga imekuwa mbovu.
    Hata mechi walizoshinda msimu huu, walishinda kwa sababu ni Yanga tu.
    Kabla ya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, nilialikwa radio Clouds kwenda kuzungumzia mchezo huo na katika tathmini yangu nilisema wazi Yanga inakwenda kufungwa, kwa sababu nilikwishaangalia tofauti ya ubora baina ya timu hizo.
    Lakini Yanga ilishinda 1-0 na siri ya ushindi ule wanayo viongozi wa Yanga, hususan Wajumbe wa Kamati ya Mashindano, ambao wengine tayari wamekwishajiuzulu akina Seif Ahmad Magari na Abdallah Bin Kleb.
    Yanga ilishinda kwa uwezo, au ni ile rekodi ya mazungumzo ya mipango ya hujuma iliyonaswa na kutumiwa kama tishio la kushinda mechi hiyo? Watu hao wanajua.
    Kile nilichokisema wakati ule Clouds, hakikutimia- ila leo kimetimia Yanga, imekula mkono. Naweza kuhisi kujiuzulu kwa akina Seif kulitokana na kusoma ishara za nyakati- nahisi tu, inawezekana pia ikawa dhamira ambayo haikuwa na shinikizo lolote nyuma yake.
    Lakini ukweli wa mambo ni huo- usanii na ujanja ulizidi kupita kiasi Yanga- na hawakujua kwamba yana mwisho hayo.
    Walijiamini zaidi  baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita katika ujanja walioutumia- lakini hawakujua ni ipi misingi mizuri ya kujenga timu imara ya ushindi.
    Ujuaji umezidi Yanga- usajili haukuzingatia maadili wala ufundi- sifa za mchezaji kiushindani hazikuzingatiwa na wachezaji wengi walisajiliwa kutoka timu ambazo zilishuka daraja au si za ushindani.
    Wesley Sneijder alikuwa kiungo gumzo msimu uliopita Ulaya na wengi walimpigia debe hadi dirisha dogo msimu huu asajiliwe Manchester United, lakini babu Sir Alex Ferguson aliona bora kumrudisha uwanjani Paul Scholes.
    Leo Sneidjer yuko wapi? Yuko inter bado, lakini anawika tena? Nini aliona Ferguson? Utaalamu tu, ambao Yanga haupewi nafasi ndiyo maana wakamrudisha Kostadin Papic.
    Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga alionekana wazi kukasimu madaraka kwa Kamati zake hasa katika sekta muhimu ya timu, kuanzia usajili na hadi uratibu wa mashindano.
    Hadi kabla ya akina Seif kujiuzulu, tayari Yanga ilikuwa imekwishapoteza nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani- lakini leo utaona Nchunga pekee ananyooshewa vidole.
    Lawama za kufanya vibaya kwa Yanga msimu huu, zinawahusu wote miongoni mwa viongozi wa Yanga, kama ambavyo walipewa sifa za kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa mipango yao.
    Lakini katika dunia ya leo, watu hawafarakani kwa sababu ya matatizo na wala hawajengi chuki za kudumu, zaidi ya kuketi chini na kujadili kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mambo.  
    Tatizo la Yanga ni uongozi usio ni mipango ya kisoka- na si kiongozi mmoja kwa sababu yanayoendelea yanaonekana. Viongozi wa Yanga wapo katika wakati mgumu hivi sasa baada ya matokeo haya- lakini wanapaswa kuonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa kutulia na kutafuta namna ya kuirudisha Yanga imara kwenye mashindano ya msimu ujao.
    Najua, kwa wengine hususan wale wapinzani wa Nchunga, kwao yametimia na wamepata sababu ya aondoke- lakini wansahau Katiba haitoi fursa ya hilo wanalolitaka wao.
    Kubwa hapa ni kurudisha umoja ndani ya klabu- viongozi waliojizulu warejee madarakani na baada ya hapo Yanga iwe moja watafute namna ya kulipa kisasi cha leo cha 5-0 na kurudisha Kombe lao msimu ujao.
    Leo ni Mei 6 na miezi miwili ijayo Yanga watakuwa na mtihani wa kutetea Kombe lao la Afrika Mashariki na Kati- unaweza kuona kuna kipindi kifupi mno cha klabu hiyo kujipanga.
    Ni kipindi kifupi, kwani matatizo ni makubwa, kwanza suala la mgogoro, pili kurudisha umoja ndani ya klabu, tena usio wa kinafiki na tatu kutengeneza timu, kuanzia kuajiri kocha na baada ya hapo kuandaa timu.
    Miezi miwili ni michache na maana yake sasa, Yanga hawapaswi kupoteza muda, mara moja waende kwenye ajenda ya kuelekea kuirudisha Yanga imara msimu ujao.
    Mkutano Mkuu ni kitu ambacho kinatakiwa mapema sana na kwa sababu gharama za mkutano zinatolewa na wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hakuna sababu ya kuchelewesha suala hili.
    Kwa sasa wawaache watani wao wa jadi wakishereheka ushindi mnono wa 5-0 na Kombe la ubingwa wa Ligi kuu, huku wakiendelea kutamba katika michuano ya Afrika- wao wamevuna walichopanda.
    Seif, Bin Kleb na Nchunga wote wanahusika na kufanya vibaya kwa Yanga msimu huu kama ambavyo wanahusika na timu kutwaa ubingwa wa Bara, Kagame, Ngao mwaka juzi na kumfunga Simba katika mechi kadhaa tangu waanze kazi.
    Matatizo mengine ya uongozi hayawezi kuwatenganisha- ndiyo maana hata rais Jakaya Kikwete anaendelea kuiongoza nchi hii na jopo lake, licha ya matatizo makubwa kila siku ambayo yamemfanya abadili Baraza la Mawaziri wiki hii tu.
    Kauli mbiu ya Yanga ni dame mbele, nyuma mwiko. Kufungwa 5-0 na Simba leo wasichukulie kama mwisho wa maisha, Yanga ilifungwa 6-0 mwaka 1977 na hadi leo bado ipo na imeendelea kujiongezea mashabiki na mataji.
    Wawe na mioyo migumu kama ambavyo walikuwa Asrenal wakati wanapigwa 8-2 na Man United hatimaye wanamaliza msimu wakiwa imara tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUBORONGA YANGA MSIMU HUU, WOTE WANAHUSIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top