![]() |
Manji |
YUSSUF Mehboob Manji,
ameibuka tena Yanga, baada ya kimya cha muda mrefu akijitokeza kwa nia ya
kuokoa jahazi kutokana hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili klabu kwa sasa.
Waajiriwa wa Yanga,
wakiwemo makocha, wachezaji na watendaji hawajalipwa mishahara kwa takriban
miezi minne, hali inayoashiria uongozi wa klabu hiyo, chini ya Mwenyekiti wake,
Wakili Lloyd Baharagu Nchunga umeelemewa.
Lakini mfanyabiashara
kijana anayemiliki mamilioni ya fedha, Manji yu tayari kuokoa jahazi kwa
kurejesha udhamini katika klabu.
Hata hivyo, ili kurejea
kuidhamini Yanga, Manji ametoa masharti matano.
Masharti hayo ni;
kufanyika uhakiki wa mahesabu ya akaunti za Yanga ndani ya siku 90 na wakaguzi
wa hesabu wa kujitegemea kukagua hesabu za kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi
2012 kwa ajili ya fedha zilizoingia klabuni.
Sharti la pili ni
kuchapishwa magazetini kwa akaunti za Yanga siku 15 baada ya kumalizika kwa
robo ya mwaka, tatu ni
kuendeshwa zoezi la
kura ya maoni ndani ya siku 60 na kuamua
kama wanachama wa Yanga wanataka klabu iwe Yanga au la na sharti la nne ni
mabadiliko ya Katiba ndani ya siku 90.
Kwa mujibu wa barua ya
Manji kwa Mwenyekiti wa Yanga, Nchunga ambayo BIN ZUBEIRY imeipata nakala yake,
ameutaka pia uongozi kuidhinisha mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu,
nafasi ambayo iko wazi baada ya Davis Mosha kujiuzulu mwaka jana.
Sharti la mwisho la
Manji ni kutaka kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa wanachama ndani ya siku 30, ili
kujadili mustakabali wa klabu.
Hii ni mara ya pili kwa
Manji tangu ajitoe Yanga, kuibuka na kutoa masharti ili arejeshe ufadhili wake,
Yanga awali mwaka jana uongozi wa Yanga, chini ya Mwenyekiti wake, Nchunga
ulimkatalia.
Ikumbukwe Februari mwaka
jana, Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga iliona ni ngumu kutekeleza masharti
manne ya Manji na kuridhia uamuzi wake wa kujitoa kwenye klabu hiyo kama
Mfadhili na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Klabu.
Chini ya Mwenyekiti
Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na aliyekuwa Makamu wake, Davis David Mosha-
historia iliandikwa, Manji alijitoa Yanga na kubaki kutekeleza mkataba wake na
klabu hiyo tu wa kuendesha vyombo vya habari vya klabu, kupitia kampuni yake ya
Quality Media Group.
Wengi miongoni mwa wana
Yanga hapana shaka watakuwa wanakumbuka kwamba, Manji alifikia uamuzi wa
kujitoa Yanga, baada ya kuona sharti lake la kutaka ukaguzi wa hesabu ufanyike
kwenye klabu hiyo, lakini ikawa inapigwa chenga na wakati huo huo wanatokea
watu wa kumchafua kutokana na kutoa sharti hilo.
Kimsingi hadi sasa
haieleweki Yanga yenye viongozi waliokwenda shule, tena wa zama za leo za
sayansi na teknolojia, kwa nini wanakwepa zoezi la ukaguzi wa hesabu za
kilichoingia na kilichotumika klabuni.
Awali, baada ya Manji
kujitoa, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nchunga alimfuata kumuomba abadilishe uamuzi
wake na aendelee kuifadhili Yanga, lakini naye akawapa masharti manne, mepesi
na yenye lengo la kuisaidia klabu hiyo.
Nitakumbusha masharti
hayo; Manji alitaka ukaguzi wa hesabu za klabu hiyo ufanyike haraka na itolewe
ripoti itakayoonyesha mapato na matumizi ya fedha zote za klabu hiyo ambazo
zimeingia kupitia vyanzo mbalimbali.
Pili, mdhamini huyo
ameitaka Kamati ya Utendaji ya Yanga kuhakikisha wachezaji wa klabu hiyo
wanalipwa fedha zao kama ilivyokubaliwa katika mikataba yao.
Sharti la tatu ni
uongozi wa Yanga kutomuingilia aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Sam Timbe katika
benchi lake la ufundi na sharti la nne ni kuifanya klabu ijitegemee.
Kufuatia masharti hayo,
Kamati ya Utendaji ya Yanga ilikutana na kuridhia Manji aondoke- maana yake
nini, masharti yake manne hayatekelezeki. Hakuna tafsiri nyingine ya uamuzi
huo, zaidi ya hiyo kwa sababu Manji alikuwa wazi na kadiri walivyoweza viongozi
wa klabu hiyo wamekuwa wazi pia.
Ni hawa viongozi
walioingia madarakani katika uchaguzi uliotawaliwa na mizengwe- tena uchaguzi
uliokosa sifa za kuitwa huru na wa haki, walifikia maamuzi mazito kama hayo.
Kwa wenye kuifahamu
vema Yanga, watakuwa wanakumbuka namna klabu hiyo ilivyopitia kwenye wakati
mgumu kiuchumi muongo uliopita kiasi cha kushuka kwa kiwango kikubwa kisoka.
Yanga ilitamba kwenye
soka ya Tanzania na Afrika kuanzia miaka ya 1960 mwishoni hadi 1970 kabla ya
mgogoro wa kihistoria mwaka 1976 ambao ulikuwa chanzo cha kuzaliwa kwa Pan
African na tangu hapo ilisota hadi mwaka 1981 ilipokuwa imara tena.
Miaka yote ya 1980
kiwango cha Yanga hakikuyumba sana na hali ikawa nzuri zaidi miaka ya 1990
baada ya kujitokeza kwa wafadhili wa Kiasia, wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa
Kilombero, Morogoro, Abbas Gulamali (sasa marehemu) na wengine kama Murtaza
Dewji aliyetokea Pan African.
Huwezi kuacha kumtaja
mtu kama Mohamed Virani ‘Babu’ aliyekuwa akiisaidia klabu hiyo tangu miaka ya
1980- enzi hizo Yanga ikimtangazia bidhaa zake kama sabuni za Bobby Soap na
soda za Vimto kwa kuvaa jezi zenye nembo ya bidhaa hizo.
Uchaguzi uliofanyika
mwaka 1993 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, uliwaingiza madarakani Dk Jabir
Katundu kama Mwenyekiti na George Mpondela ‘Castro’ kama Katibu Mkuu na hawa
walijaribu kwa mara ya kwanza kutaka kuifanya Yanga ijitegemee.
Mfanyabiashara Reginald
Mengi alikuwa tayari kuisaidia Yanga kutekeleza azma ya klabu kuwa kampuni,
lakini zikatokea hujuma tu za watu wenye kupenda kuona klabu hiyo inabakia kuwa
kama ilivyo, ili waendelee kutimiza mambo yao.
Zoezi hilo lilikwama na
ukatokea mgogoro mkubwa tena Yanga, hata viongozi wakaondoka madarakani kabla
ya kumaliza muda wao- wafadhili nao wakaingia mitini wote.
Hadi Rashid Ngozoma
Matunda (sasa marehemu) anachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu mwaka 1996,
Makamu wake, Mohamed Namanganya (sasa marehemu), Katibu Mkuu wake Frank Mutani,
Yanga ilikuwa iko vibaya kiuchumi.
Uongozi huu ulipata
misukosuko mingi, kwanza kashfa za ubadhirifu za viongozi wenyewe kwa wenyewe
zilizomfanya Mutani akaachia ngazi- baadaye hali ngumu ndani ya timu hadi
wanachama wakakasirika na kuanza kuutia misukosuko uongozi huo- walikuwa
wakiupindua kila siku na kuweka Kamati za Muda.
Nakumbuka Salim
Ngereza, Tarimba Abbas- kwa wakati tofauti hawa walikuwa Wenyeviti wa Kamati za
Muda Yanga, katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2000, wakati huo bado uongozi
unaotambulika Kikatiba ni wa Matunda.
Hatimaye mwaka 2000
akina Tarimba wakafanikiwa kumtoa Matunda na kuifanya klabu kuwa kampuni,
ingawa ilikuwa kampuni jina. Lakini kundi la wana Yanga wengine likiongozwa na
Yussuf Mzimba liliingia msituni na kuanzisha kitu kinaitwa Yanga Asili,
likiipinga Yanga Kampuni.
Mgogoro uliendelea na
hali ikazidi kuwa mbaya, hatimaye mwaka 2003 Tarimba akaondoka kwenye klabu
hiyo, Mbaraka Igangula akakaimu na baadaye ukafanyika uchaguzi wa Yanga
Kampuni, Francis Kifukwe akawa rais wa klabu.
Wakati wote huo hali
ilikuwa ni ngumu Yanga, klabu haina mfadhili- baada ya kupitia kwenye mikono ya
udhamini wa Mobitel (sasa Tigo) na Shivacom kwa muda mfupi, fedha za mkononi za
viongozi zikiihudumia timu.
Hiki ndicho kipindi
ambacho Yanga ilikuwa inaacha madeni kwenye hoteli mikoani ilipokwenda kucheza
mechi zake za Ligi na kufika mwaka 2006 hali ilikuwa ngumu zaidi, hadi
kikajitokeza kikundi cha wana Yanga kisichofungamana na upande wowote kuamua
kuchangisha fedha za kuisaidia timu ikiwa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, mjini Dar es Salaam.
Mkutano ulifanyika
kwenye ukumbi wa Reli Gerezani Club na kuanzisha harambee ya Saidia Yanga. Hapo ndipo walipojitokeza watu kutoa namba za
matajiri maarufu nchini wanaowafahamu fika ni wapenzi au wanachama wa Yanga na
katika staili hiyo alipatikana Manji.
Manji alijitolea kwa
moyo mmoja kuisaidia klabu hiyo na akasema pia angependa umoja ndani ya klabu,
akaingia gharama kubwa kusuluhisha mgogoro wa Yanga Asili na Yanga Kampuni na
hatimaye mwafaka ukapatikana na ukasainiwa na pande zote mbili, kwa makubaliano
maalum.
Mei mwaka 2007
ukafanyika uchaguzi wa kwanza halali Yanga, tangu ule wa mwaka 1996 uliomuweka
madarakani marehemu Matunda na timu yake. Katika uchaguzi huo wa 2007, Wakili
Imani Omar Madega akashinda Uenyekiti, Ngozoma Matunda makamu wake, Katibu Mkuu
Lucas Kisasa.
Kwa kuwa yaliyofikiwa
kwenye mwafaka hayakutekelezwa, ikiwemo timu kukabidhiwa kwa kampuni na akina
Madega wakabaki kuwa viongozi wa klabu, hali haikuwa shwari moja kwa moja
Yanga, mivutano iliendelea, Manji akisisitiza klabu kujitegemea kwa kuwa na
kampuni ya kuuza hisa, tena akitoa michanganuo ya kitaalamu, inayoainisha jinsi
ambayo klabu hiyo itanufaika.
Manji ameingiza fedha
nyingi Yanga tangu mwaka 2006, nyingine zilikuwa ni za matumizi yasiyokuwa na
maana, kama kusaidia matawi sijui- labda kwa lengo la kuwafurahisha wanachama,
lakini hazikuisaidia klabu.
Umefika wakati anataka
kuona fedha zake zinaisaidia Yanga moja kwa moja na kutaka kuiwezesha klabu
ijitegemee, lakini watu wanaleta vikwazo kiasi cha kufikia uamuzi wa kusema;
Acha aende.
Nimeeleza namna Manji
alivyopatikana Yanga, haikuwa kazi rahisi na klabu ilipitia msoto wa muda
mrefu, sijui wakati huo akina Nchunga na Mosha walikuwa wapi- walikuwa hawajui
klabu ilivyokuwa inataabika? Na mbona hawakujitokeza wakati huo?
Mwana Yanga wa kweli,
daima lazima ataweka mbele maslahi ya klabu yake na kama hilo lingezingatiwa,
Manji asingeondoka Yanga.
Suala si Manji, bali ni
mustakabali wa klabu baada ya Manji, kwani Yanga ya leo si ile ya miaka 10
iliyopita, mambo yamebadilika mno, ikiwemo bajeti ya uendeshwaji wake, kuanzia
mishahara ya wachezaji na makocha.
Tunaona sasa katika
kipindi ambacho Manji amekuwa nje Yanga, hali imekuwa ngumu, wachezaji wanalia
njaa, usajili wa kisanii ulishaanza, mchezaji anasaini makaratasi bila kupewa
fedha sasa.
Inafikia wachezaji wanagoma
kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara na pia wanalalamikia maji hayapandi juu
klabuni.
Hii ni safari ya klabu kurudi
kule kule ilipotokea kwenye kutembeza mabakuli jukwaani kuchangisha fedha za
kuhudumia timu, lakini ‘Mungu saidia’, Manji karudisha moyo wake nyuma na kutaka
masharti yake yatekelezwe naye arejeshe udhamini wake klabuni.
Mimi nastaajabu kitu
kimoja, Yanga ni taasisi kubwa ambayo ipo kwa mujibu wa sheria- serikali
inaitambua Yanga kama si mali ya mtu ni ya wananchi. Hofu ya Yanga kugeuzwa
Kampuni inatoka wapi?
England pale timu zote
kubwa sasa zinaendeshwa na wageni, lakini bado wapenzi na mashabiki wake ni
wale wale, zaidi wamenufaika kwa kufanyiwa klabu zao ziwe bora zaidi na zenye
hadhi ya mwonekano na mafanikio.
Miaka mitano iliyopita
nani alikuwa shabiki wa Manchester City nje ya Manchester tu pale? Mimi sielewi
hofu inatoka wapi na hasa linapokuja suala la ukaguzi wa hesabu watu wanapiga
chenga, hii inaashiria nini?
Kwa nini sasa Nchunga
asikubaliane na masharti ya Manji- kwani ni mepesi tu na kimsingi suala la
kujazwa kwa nafasi ya Mosha au mabadiliko ya Katiba ni muhimu, ili kupata
Katiba bora zaidi kwa manufaa ya klabu, mbona ni masuala yanayowezekana?
Au Nchunga anahisi nini
nyuma ya masharti haya- na kama kuna hatari yoyote basi awaeleze wana Yanga
wajue, lakini kinyume chake ataonekana yeye ndiye tatizo.
Mimi sioni tatizo
katika masharti ya Manji na yeyote mwenye mlengo wa maendeleo na kutaka kuiona
Yanga ya kisasa- sidhani kama anaweza kutofautiana nami. Alamsiki.
0 comments:
Post a Comment