![]() |
| Kiiza wa Yanga kushoto akitafuta mbinu za kumtoka Nassor Masoud Chollo wa Simba katika mechi iliyopita baina ya timu hizo, miamba hiyo sasa itacheza Jumapili badala ya Jumamosi. |
KIKAO cha Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bata leo
kimepanga mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar ichezwe kesho Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, wakati mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, iliyokuwa ifanyike
Jumamosi sasa imesogezwa mbele hadi Jumapili.
Azam na Mtibwa Sugar wanarudiana kesho jioni Uwanja wa Taifa,
kufuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana jana.
Kamati ya Tibaigana, Kamanda Mstaafu wa Jeshi la Polisi,
Kanda Maalum, Dar es Salaam, jana ilibatilisha maamuzi ya Kamati ya Ligi Kuu,
kuipa Azam ushindi, baada ya kuvunjika mechi yao na Mtibwa wiki iliyopita,
zikiwa zimebaki dakika chache mchezo kumalizika na kuamuru mechi irudiwe.
Kamati ya Tibaigana ilibaini mapungufu kwa marefa wa mechi
hiyo, kwani hawakufuata kanuni za mchezo kusubiri kwa dakika 10 kabla ya
kumaliza mechi hiyo, baada ya Mtibwa Sugar kugomea penalti timu hizo zikiwa
zimefungana bao 1-1.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia ameiambia BIN
ZUBEIRY jioni hii kwamba kwa sababu walipanga mechi zote za mwisho za ligi zichezwe
siku na wakati mmoja Jumamosi, kutokana na Azam na Mtibwa kuwa na mechi kesho,
hawataweza kucheza siku mbili mfululizo.
Kwa sababu hiyo, Karia amesema Kamati imeamua mechi za
mwisho zote, ikiwemo ya watani wa jadi Simba na Yanga sasa zichezwe Jumapili,
ili kuzipa nafasi ya kupumzika siku moja Azam na Mtibwa kabla ya kuingia kwenye
mechi zao za mwisho.



.png)
0 comments:
Post a Comment