![]() |
Okwi akishangilia moja ya mabao yake. picha hisani ya Full Shangwe |
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC jioni hii
wamekabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe
nzito, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuwabwaga wapinzani wao
wa jadi, Yanga mabao 5-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
Hiki ni kipigo cha pili kihistoria Simba
wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
Ilikuwa ni hoi hoi, nderemo na vifijo
kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi
nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala na shangwe za Simba.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele
kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel
Arnold Okwi dakika ya kwanza tu ya mchezo huo.
Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko
baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
Katika kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita
kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye
aliishia kumkwatua mara kwa mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha
kupumzikia akiwa ana kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga
waliendelea kucheza kwa utulivu, wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi
kadhaa, ingawa kikwazo kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
Nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho na
ambayo Yanga wataijutia waliipata dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa
Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye
na kipa, hesabu zake ziliendana na Kaseja.
Kiiza aliupelekea mpira upande wa kushoto
wa kipa huyo bora Tanzania, ambaye naye akachupa upande huo huo na kuokoa.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa
mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati
Simba walimpumzisha Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa
mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
Bao la pili la Simba lilitokana na penalti,
baada ya Nsajigwa Shadrack kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu
akaenda kufunga kwa penalti.
Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 52,
baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro
alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina.
Dakika ya 66 Uhuru Suleiman aliangushwa na
Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti.
Patrick Mafisango alifunga bao la tano kwa penalti
pia dakika ya 73.
Simba SC: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’,
Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa,
Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher,
Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Yanga: Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa
Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth
Asamoah, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
kufanya makosa katika eneo la hatari
Mchezaji wa Simba Emmanuel Okwi akiwania mpira mbele ya Shadrack Nsajigwa wa Yanga katika mchezao wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania inayomalizika leo.
Mashabiki wa timu ya Simba wakishangilia timu yao.
Mashabiki wa timu ya Yanga wakiangalia kitu jukwaani haikufahamika lilikuwa ni tukio gani.
Wachezaji wa timu za Simba na Yanga wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mchezo huo kwenye uwanja wa Taifa.
Kikosi cha timu ya Simba ambao ndiyo mabingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2011-2012 kikiwa katika picha ya pamoja na Kocha wao Milovan.
Manahodha wa Simba na Yanga Juma Kaseja kushoto na Shadrack Nsajigwa wakisalimiana mbele ya waamuzi kabla ya kuanza kwa mpambano huo.
Mashabiki wa timu ya Simba wakiwa wamefurika uwanjani hapo.
0 comments:
Post a Comment