KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) imepanga vituo vitatu vya Ligi ya Taifa inayoshirikisha
mabingwa wa mikoa kwa ajili ya ligi hiyo itakayoanza Mei 26 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba Kundi A
lenye mabingwa wa mikoa ya Iringa (Kurugenzi Mufindi), Lindi (Lindi SC), Mbeya
(Tenende FC), Morogoro (Mkamba Rangers), Mtwara (Ndanda SC), Pwani (Super
Star), Rukwa (Mpanda Stars) na Ruvuma (Mighty Elephant) zitacheza mechi zake
mjini Mtwara.
Amesema Mji wa Kigoma utakuwa mwenyeji wa
mabingwa wa mikoa ya Dodoma (CDA), Kagera (Bandari FC), Kigoma (JKT Kanembwa),
Mwanza (Pamba SC), Shinyanga (Mwadui SC), Singida (Aston Villa) na Tabora
(Majimaji).
Amesema Kundi C lenye mabingwa wa mikoa ya
Arusha (Flamingo SC), Dar es Salaam (Ashanti United ya Ilala, Red Coast ya
Kinondoni na Tessema FC ya Temeke), Kilimanjaro (Forest FC), Manyara (Nangwa
VTC), Mara (Polisi Mara) na Tanga (Korogwe United) watachezea mechi zao mkoani
Mara.
Amesema mwisho wa kuwasilisha fomu za
usajili ni Mei 15 mwaka huu wakati kipindi cha pingamizi ni kuanzia Mei 16 hadi
22 mwaka huu. Mei 23 mwaka huu Kamati ya Mashindano ya TFF itakutana kupitia
usajili huo. Wachezaji wanaosajiliwa ni wale wale waliochezea timu hizo katika
ligi ya mkoa.
Amesema Mei 14 mwaka huu ni mwisho kwa
mikoa yenye pingamizi kwa mabingwa wao kuwa wameshashughulikia rufani husika.
Kamati ya Mashindano imeagiza kuwa kwa mikoa itakayoshindwa kufanya hivyo mpaka
baada ya tarehe hiyo mabingwa wao hawatashiriki ligi hiyo.
Amesema timu tano zitapanda daraja kucheza
Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao. Mshindi wa kwanza kutoka kila kundi na
washindwa wawili bora (best losers) kutoka kundi A na C ambayo yana timu nane
kila moja.
Wakati huo huo: Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa
mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia 2014 Kanda ya Afrika kati ya Lesotho na Sudan
itakayochezwa jijini Maseru.
Wambura amesema mechi hiyo ya kwanza ya
raundi ya pili itachezwa kati ya Juni 1 na 3 mwaka huu. Lesotho na Sudan ziko
kundi D pamoja na Ghana na Zambia.
Naye Hafidhi Ally ameteuliwa na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa Kamishna wa mechi ya Ligi ya Mabingwa
Afrika kati ya Dynamos FC ya Zimbabwe na Esperance Sportive ya Tunisia.
Mechi hiyo ya marudiano hatua ya 16 bora
itachezwa Mei 13 mwaka huu kwenye Uwanja wa Rufaro jijini Harare. Esperance
Sportive ilishinda mechi ya kwanza kwa mabao 6-0.



.png)
0 comments:
Post a Comment