![]() |
Na Mahmoud Zubeiry |
NI katika makala yangu iliyopita, nilipowaambia Yanga,
kwamba kusajili wachezaji wazuri siyo kuwa na timu nzuri na ni jana tu
lilipodhihirika hilo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati timu hiyo ilipokuwa
ikimenyana na Express ya Uganda katika mchezo wa kirafiki.
Pamoja na Yanga kushinda mabao 2-1, lakini mapungufu makubwa
yalionekana- kubwa timu haichezi kwa muundo (formation) wenye kueleweka, haina
mipango kabisa, ingawa kweli wachezaji walikuwa wakionana uwanjani.
Kuna mambo mawili ambayo yanawatatiza mashabiki wengi wa
soka nchini- kwanza kucheza kwa uelewano na pili wachezaji kuonana uwanjani.
Kucheza kwa uelewano kunatokana na muundo, ambao unatokana
na mafundisho ya mwalimu- lakini wachezaji kuonana uwanjani na kupeana pasi ni
jambo ambalo linaweza kufanywa na timu yoyote, hata isiyo na mwalimu ili mradi
tu wanajijua wanacheza dhidi ya wapinzani.
Siyo kila kugongena pasi, basi ni timu kucheza kwa uelewano-
hapana na kwa sasa hicho ndio kitu ambacho Yanga inakosa. Yanga wamegonga pasi
jana, lakini zilikuwa za kupoteza muda tu kwa sababu hazikuwa na dhamira yoyote
iliyoonekana.
Lakini wachezaji bado hawana pumzi na stamina ya kutosha-
ndiyo maana walitawala mchezo kwa dakika 45 tu za kwanza, lakini kipindi cha
pili mambo yalikuwa magumu upande wao.
Muundo; Yanga lazima wawe na namna yao ya kucheza katika mpangilio,
wakijua wanaanzaje katika kuelekea eneo la wapinzani hadi kupata bao.
Yanga lazima wawe na uelewa na mbinu za kukaa na mpira kwa
muda mrefu mchezoni bila kupoteza, ili kupunguza makali ya wapinzani.
Yanga lazima wawe na mipango ya kuwahadaa wapinzani wa aina
yoyote, iwe wenye kushambulia au kupaki basi.
Yanga lazima wawe na mipango ya kutengeneza nafasi, lazima
wawe na mipango ya kutumia hizo nafasi wanazopata pia. Haiwezekani timu inapiga
kona nane, bila bao hata moja.
Haiwezekani Yanga wanapiga mipira ya adhabu zaidi ya mitano
nje ye eneo la mita 18, bila ya kulenga lango.
Niwapongeze kwa mabao mawili waliyopata jana yalitokana na
mipira ya pembeni na katika soka ya dunia ya leo, mbali na mipira ya adhabu
mabao mengi hutokana na mipira ya pembeni.
Lakini haikutokana na mipango zaidi ya uwezo binafasi wa
wachezaji wake bora iliyowasajili tena wote waliocheza jana walikuwa wazawa-
faraja iliyoje na unaweza kuiona timu bora ya taifa ya baadaye ikiundwa na
wachezaji wa Yanga.
Ni kweli, Yanga inasifiwa kufanya usajili mzuri kwa ajili ya
msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, miongoni mwa wachezaji
iliyowasajili wakiwemo Kelvin Yondan, Ally Mustafa ‘Barthez’ kutoka Simba na
Frank Damayo kutoka JKT Ruvu.
Kulingana na hali halisi ya uwezo wa wachezaji hao kwa sasa,
hususan Yondan, wenyewe wanamuita Vidic na Damayo, mashabiki wa Yanga
wamesuuzika mno na nafsi zao. Wanaamini wachezaji hao na wengineo, wataifanya
timu yao iwe tishio msimu ujao.
Jerry Tegete anampiga tobo kipa wa Express, Didi Mahmoud kufunga bao la kwanza jana |
Yanga sasa wana ndoto nyingi sana juu ya timu na japokuwa
mwakani hawatashiriki michuano ya Afrika, lakini wanaona kabisa wamekwishatetea
Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Yanga tayari wa ndoto za kulipa zile 5-0 walizopigwa na
watani wao wa jadi, Simba msimu huu. Wanaota kurejesha ubingwa wao wa Ligi Kuu
na kwa ujumla heshima yao katika soka ya Tanzania, waliyoipoteza msimu
uliopita.
Kwa ujumla wana matumaini makubwa sana, hasa wakizingatia
Mwenyekiti wao atakuwa Yussuf Manji, Makamu wao Mwenyekiti Clement Sanga na
Wajumbe kama Abdallah Bin Kleb, Peter Haule na wengineo- wana Yanga, wana
matumaini makubwa sana na kikosi chao kipya.
Lakini pamoja na ukweli huo, bado nasistiza Yanga wanatakiwa
kutambua kwamba; Kusajili wachezaji wazuri ni suala moja na kuwa na timu nzuri
ni suala lingine.
Yanga wamefanikiwa mtihani wa kusajili wachezaji wazuri, na
sasa wanatakiwa wapitie katika zoezi gumu zaidi la kutengeneza timu nzuri ya
ushindani kwa mashindano ya ndani na nje.
Bahati nzuri, Yanga wana muda wa kutosha kwa sababu msimu
wote ujao utakuwa wa kutengeneza tu timu yao kwa kuwa hawashiriki michuano ya
Afrika- hivyo kama watafanikiwa kufuzu na mtihani huo pia, tegemea kabisa Yanga
ya 2014 itakuwa tishio hadi Afrika.
Lakini hiyo timu nzuri inatengenezwaje? Kwanza kuwa na
mwalimu bora, atakayepeta fursa na wasaa mzuri na wa kutosha wa kuwaandaa
wachezaji. Haitoshi tu kusajili wachezaji wazuri na kisha unawakabidhi kwa
msimamizi wa mazoezi, ni hatari kwa vipaji vyao.
Yanga wanatakiwa kutengeneza sera nzuri za benchi la ufundi,
ambalo litakuwa na nguvu na kuheshimiwa na wachezaji, tofauti na ilivyo hivi
sasa, mchezaji anamuheshimu Seif Magari, anamdharau Freddy Felix Minziro.
Yanga inatakiwa kuwa wazi kwa wachezaji wake, kuwaambia
imewasajili kwa ajili ya kufanya kazi na wasilewe sifa na kuanza kupandisha
mabega juu, uwanjani hawajitumi, matokeo yake wanarudi kule kule, kwenye
kununua mechi.
Haiwezekani, usajili huu wa Yanga naomba niseme mapema
ulikuwa makini mno, tofauti na usajili wa miaka miwili, mitatu iliyopita na timu
iliyopewa jukumu hilo, ililifanikisha kwa umakini wa hali ya juu.
Kwa sababu hiyo basi, wachezaji lazima wacheze soka
uwanjani, watengeneze matokeo mazuri kwa uwezo wao. Wadumishe viwango vyao, ili
waendelee kuwapo timu ya taifa. Lakini kubwa na la msingi ni mashabiki wa Yanga
kuwa na subira kabla ya kupata timu nzuri.
Yanga watawaona wachezaji wao wazuri katika Kombe la Kagame
na watafanya sana vitu adimu binafsi na ikibidi, kweli watatetea hadi Kombe
lao- lakini kuwa na timu nzuri kwa maana ya timu inayocheza soka ya kuelewana,
iliyotokana na mafundisho, wana Yanga wanatakiwa kuwa na subira.
Vema imekwishaelezwa kocha kutoka Ubelgiji wamekwishafikia naye
makubaliano na atatua wakati wowote nchini kuanza kazi.
Kama atakuwa mwalimu mzuri, naamini wakimpa fursa na wasaa
mzuri na wa kutosha, kuanzia mzunguko wa pili Yanga itakuwa inacheza ‘kitenisi’
cha kutisha- ila kama ubabaishaji utaendelea na hakutakuwa na sera nzuri za
benchi la ufundi, mafunzo, nidhamu na kujali maslahi ya wachezaji, basi
wachezaji hawa Desemba tu wataonekana hawafai.
Simon Msuva kulia |
Nataka nimalizie kwa kuwaambia Yanga, wapeleke timu ya
kambini, waepuke mechi za kirafiki zilizo nje ya program ya walimu, watumie
vizuri wiki mbili hizi zilizobaki kabla ya kuanza kwa Kombe la Kagame. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment