![]() |
| Nassor Bin Slum na kijana wake |
Na Princess Asia
MFADHILI Mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Nassor Bin Slum amesema kwamba, Wagosi hao wa Kaya watakuwa tishio katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na usajili mzuri waliofanya.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Nassor ambaye pia ni mfadhili wa Villa Squad ya Kinondoni, alisema kwamba uongozi wa Coastal ulikuwa makini na wenye utulivu wa hali ya juu katika zoezi la usajili, kuhakikisha kwamba wanasajili wachezaji watakaorejesha hadhi ya timu hiyo, iliyokuwa tishio siku za mwanzoni za soka ya Tanzania.
“Mchezaji kama Razack Khalfan, huyu ni bora kabisa mwenye kiwango cha kucheza timu ya taifa, huwezi kupata sababu kwa nini Yanga walimuacha, ila msimu ujao watamuona. Bado kuna wanaume wengine wa shoka kibao tumesajili, kwa kweli msimu ujao tutatisha,”alisema Nassor.
Mabingwa hao wa 1988, tayari wamekamilisha usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wametaja kikosi chao, kupitia facebook page yao.
Kikosi cha Coastal msimu kitaundwa na makipa; Juma Mpongo, Abraham Chove na Rajab Kaumba, mabeki; Said Sued (Nahodha) Mbwana Kibacha (Nahodha Msaidizi) Othman Omary, Juma Jabu, Ismail Suma, Jamal Machelenga, Cyprian Lukindo na Philipp Mugenzi.
Viungo watakuwa ni Jerry Santo, Razack Khalfan, Mohamed Binslum, Khamis Shango, Mohamed Issa, Mohamed Soud, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Lameck Dayton, Joseph Mahundi, Aziz Gilla na Shaffih Kaluani, wakati washambuliaji ni Nsa Job, Atupele Green, Danny Lianga na Pius Kisambale.
Kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Mkuu, mshambuliaji wake wa zamani, Juma Mgunda, atakayekuwa akisaidiwa na beki wa zamani wa Pan African, Habibu Kondo, kocha wa viungo, mchezaji wake wa zamani, Ally Jangalu na kocha wa makipa Bakari Shime.
Msimu ujao, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, mkoa wa Tanga utakuwa na timu mbili Ligi Kuu, zaidi ya Coastal nyingine ni Mgambo FC iliyopanda msimu huu, hivyo kukumbushia enzi zile zile za African Sports ‘Wanaq Kimanumanu’ na Wagosi hao wa Kaya.



.png)
0 comments:
Post a Comment