![]() |
| Simba SC |
Na Princess Asia
KIKOSI kizima cha wachezaji wa Simba SC, leo kinatarajiwa kutembelea Wadi ya Wazazi ya hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam katika mfululizo wa Wiki ya Simba na Jamii, kuelekea tamasha la kuazimisha kuzaliwa kwa klabu hiyo, Simba Day, Agosti 8, mwaka huu.
Katika ratiba ya Wiki ya Simba na Jamii, jana walikuwa wanatembelea kituo cha watoto yatima cha Maungu Orphanage Center, kilichopo Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam
Wachezaji wa Simba, wanatarajiwa kujumuika na wagongwa, ili kuwafariji sambamba na kuwapa zawadi mbalimbali.
Kesho ndio kilele cha Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na tamasha hilo, litatatanguliwa na burudani mbalimbali, litafuatiwa na utambulisho wa wachezaji wote wa kikosi cha msimu ujao cha Simba SC wakiwemo Mrisho Khalfan Ngassa aliyesajiliwa kutoka Azam FC, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda na wengineo.
Baada ya utambulisho, Simba itacheza mechi ya kirafiki na Nairobi City Stars ya Kenya na keshokutwa Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani, ambayo BIN ZUBEIRY na mastaa wengine kibao bongo kama Rashid ‘Snake Boy’ Matumla wamesoma ili kuhamasisha michezo mashuleni.
Wiki ya Simba na Jamii itahitimishwa kwa ziara ya kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kilichopo Ilala, Dar es Salaam, Agosti 10.
TBL ndio wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager, ambayo pia ndio imedhamini Wiki nzima ya Simba na Jamii, kuanzia kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu hiyo, Jumapili Bwalo la Maofisa wa jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam,
RATIBA YA WIKI YA SIMBA NA JAMII:
Agosti 5, 2012: Mkutano Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi Oystrebay)
Agosti 6, 2012: Kutembelea watoto yatima Maungu Orphanage Center, K’ndoni Mkwajuni
Agosti 7, 2012: Kutembelea wagonjwa Mwananyamala hospitali
Agosti 8, 2012: Simba Day (Uwanja wa Taifa, burudani na mechi)
Agosti 9, 2012: Kutembelea shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni
Agosti 10, 2012: Kutembelea kiwanda cha TBL Ilala



.png)
0 comments:
Post a Comment