![]() |
Mh Mgimwa |
Na Mahmoud Zubeiry, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Mahmoud Mgimwa
amemtaka Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji kufanya lolote analoweza, lakini
ahakikishe Simba SC inafungwa 6-0 ili kuwanyamazisha wapinzani wao hao wa jadi,
wanaotambia ushindi wa 5-0 katika msimu uliopita wa Ligi Kuu.
Mgimwa alitoa ombi hilo, wakati akitoa maoni yake kwa uongozi
wa klabu hiyo jana katika ukumbi mdogo wa Bunge mjini Dodoma, wakati wa hafla fupi
ya uzinduzi wa Tawi la Yanga Bungeni.
“Kwa kweli mimi kilio changu ni kimoja tu, Yanga sasa hivi
hatuna raha, zile 5-0 tulizofungwa hata tufanye nini, zinatuumiza, mimi
nakuomba Mwenyekiti, fanya unavyoweza na jeshi lako, kuhakikisha tunawafunga
6-0 wale ili tuheshimiane,”alisema.
Mbali na kufungwa 5-0 msimu uliopita, Yanga pia iliwahi
kufungwa 6-0 na Simba mwaka 1977.
Jana Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambao ni
wapenzi wa Yanga waliafiki kuchangia Sh. 500,000 kila mwaka katika kuchangia
maendeleo ya klabu hiyo, katika hafla fupi ya uzinduzi wa Tawi la Yanga
Bungeni.
Hiyo ilifuatia ombi la Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la
klabu ya Yanga, Mama Fatuma Karume, mke wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati
Abeid Amaan Karume leo wakati akizindua tawi la Yanga Bungeni.
Mama Karume alizindua mfuko huo kwanza yeye mwenyewe kutoa
Sh. 500, 000 ambazo zilipokewa na Mweka Hazina wa Tawi la Yanga Bungeni, Martha
Moses Mlala, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Singida.
Wabunge wengine waliotoa fedha zao hapo hapo ni Abbas Mtemvu
(Temeke, CCM). Athumani Mfutakamba (Igalula, CCM) na Grace Kiwelu (Viti Maalum,
CHADEMA).
Awali, akisoma taarifa ya tawi hilo, Mwenyekiti Misanga
ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga miaka ya 1970, chini ya Mwenyekiti
Juma Shamte, alisema kwamba Julai 31 walifanya uchaguzi wa viongozi wa tawi la
klabu hiyo Bungeni na mbali ya yeye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, Abadallah
Ameir alichaguliwa kuwa Makamu wake.
Alisema Nafasi ya Katibu Mkuu, ilikwenda kwa Godfrey Zambi,
Katibu Msaidizi, Grace Kiwelu, Mweka Hazina Martha Mlala na Wajumbe wa Kamati
ya Utendaji, Abbas Mtemvu, Halima Mdee, Victor Mwambalaswa, Mohammed Chambo,
Abdul Marombwa, Vicky Kamatta na Ritta Kabati.
Aidha, alisema waliteua pia Kamati ya Ushauri ya Wajumbe
wanne, ambao ni George Mkuchika, Zarina Madabida, Faki Makame na Chirtopher
Chiza.
Pamoja na hayo, Misanga aliupongeza uongozi mpya wa Yanga
chini ya Mwenyekiti wake Manji, na kuutaka uwe makini na wanachama wapandikiza
sumu za migogoro klabuni.
0 comments:
Post a Comment