• HABARI MPYA

    Tuesday, August 07, 2012

    YANGA WAREJEA DAR LEO

    Kikosi cha Yanga bungeni jana na Waziri Mkuu 

    Na Mahmoud Zubeiry, Dodoma
    MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya Dar es Salaam leo wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam, kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jana kuonyesha Kombe lao ubingwa wa michuano hiyo, maarufu kama Kombe la Kagame katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma.
    Yanga walifika hapa juzi, kwa mwaliko wa Tawi la Yanga Bungeni mjini hapa na baada ya shamrashamra za jana, timu inarejea Dar es Salaam.
    Jana, Mheshimiwa Spika, Mama Anna Makinda baada ya kumaliza kikao cha asubuhi alianza kutambulisha wageni mbalimbali waliotembelea Bungeni na ukumbi wa Bunge uliripuka kwa shangwe nzito, alipofikia kuwatambulisha mabingwa hao wa Kagame.
    Mama Anna Makinda, alianza kwa kuwatambulisha viongozi wa Yanga, Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Mama Fatuma Karume, Francis Kifukwe na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe wengine kabla ya kukiinua kikosi kizima wafalme wa soka kwa nchi 12 barani Afrika.
    Wakati wa zoezi hilo, Wabunge ambao ni wapenzi wa Simba, mahasimu wa jadi, wa Yanga, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wekundu hao wa Msimbazi, Alhaj Ismail Aden Rage, walianza kuwabeza wapinzani wao hao, kwa kuwakumbushia kipigo cha mabao 5-0 walichowapa katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu.
    Lakini hiyo haikuzuia sherehe za Yanga kuendelea hadi nje ya ukumbi wa Bunge, ambako Wabunge na Mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda walipiga picha na wachezaji, viongozi na Kombe lao hilo.
    Wabunge wengine na Mawaziri, ambao ni wapenzi wa Simba wakiwemo Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makala, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azam na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia nao pia walijumuika kupiga picha na Yanga.  
    Baada ya hapo, wachezaji wa Yanga na viongozi walikwenda kwenye ukumbi mdogo wa Bunge kukutana na Uongozi wa Tawi la klabu hiyo, Bungeni chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed Hamisi Misanga uliochaguliwa Julai 31, mwaka huu ambako huko Mama Karume alizindua rasmi tawi hilo.
    Yanga, waliotwaa Kombe hilo mara mbili mfululizo sasa, wachezaji wake waliwasili usiku wa juzi na baadhi ya viongozi, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Titus Osoro, Mohamed Bhinda na George Manyama pamoja na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa na Meneja, Hafidh Suleiman, wakati Mwenyekiti, Yussuf Manji na Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe wengine waliwasili jana.
    Kwa upande wa timu, wachezaji walifika pia juzi na makocha wasaidizi, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani Samatta, wakati kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet alikuja jana pamoja na viongozi hao wakuu na Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Francis Mponjoli Kifukwe na Mama Fatuma Karume.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAREJEA DAR LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top