![]() |
Redondo |
Na Prince Akbar
SIMBA wamejishitukia juu ya ‘madudu’ waliyofanya kwa kumsajili kiungo Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ jana kutoka Azam FC, bila kuwasiliana na klabu yake kujua kama ana mkataba au la.
Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo akarejea Azam.
Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Redondo bado ana mkataba na Azam na kutokana na kitendo cha Simba kufanya mazungumzo hadi kumsainisha mchezaji mwenye mkataba na klabu yake, sasa wanataka kuchukua hatua ili kukomeshsa vurugu katika usajili Tanzania.
Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na mkataba na Simba SC.
Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao yuko huru, aichezee Yanga.
Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka miwili na Yanga.
0 comments:
Post a Comment