• HABARI MPYA

    Monday, August 13, 2012

    KIM POULSEN AWATEMA KAPOMBE, DIDA STARS

    Kocha Kim kushoto akizungumza. Kulia Katibu wa TFF, Angetile

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amewaacha katika kikosi chake kinachoondoka alfajiri ya kesho kwenda Botswana katika mchezo dhidi ya wenyeji Jumatano, wachezaji wawili, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na beki Shomary Kapombe kwa sababu ni majeruhi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY usiku huu kwenye kambi ya timu hiyo, hoteli ya Somaiya eneo la Gerezani, Dar es Salaam, kocha Kim alisema anasikitika hatakuwa nao wachezaji hao kwenye safari kwa sababu ya majeruhi.
    Lakini Poulsen alisema anaamini wachezaji anaokwenda nao wanaweza kumpa ushindi katika mchezo huo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa sababu amewaandaa vizuri na wameonyesha wako tayari.
    Kim alisema Botswana ni timu nzuri na kwa sasa iko juu ya Tanzania kiuwezo, hivyo kama wakishinda utawasaidia kupanda kwenye viwango vya FIFA.
    Kim aliwataja wachezaji watakaoondoka alfajiri ni makipa; Juma Kaseja na Mwadini Ally, mabeki; Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Amir Maftah, Erasto Nyoni, viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Shaaban Nditi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Damayo, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa na washambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, Simon Msuva na Said Bahanuzi.
    Kim amesikitika kumkosa mshambuliaji Mbwana Ally Samatta katika kikosi chake, kwa sababu klabu yake Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) haijamruhusu.
    “Ni kwa sababu ya siasa kati ya klabu ya Mazembe na TFF, nasikitika kumkosa Samatta, ila sina jinsi,”alisema.
    Kim atamkosa pia mshambuliaji mwingine, John Bocco ‘Adebayor’, ambaye amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini katika klabu ya Super Sport United ya Ligi Kuu ya huko.
    Wachezaji watatu kati ya anaokwenda nao Botswana kesho, Damayo, Singano na Msuva watajiunga na timu hiyo kambini usiku huu, wakitokea Nigeria walipokuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
    Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah amewataka wachezaji wa Stars kwenda kucheza vizuri huko ili wazivutie klabu za Kusini mwa Afrika ziwasajili kwa kuwa zina maslahi makubwa kuliko hapa nchini.
    Angetile alisema kwamba Botswana ni nchi ambayo zamani ilikuwa inasajili wachezaji wa Tanzania, hivyo katika mchezo huo kama wachezaji wa Stars wataonyesha soka safi, wanaweza kuzivutia klabu za huko na zikawasajili.
    Ngassa na Yondan kulia


    Kazimoto na Maftah kulia

    Nyoni na Redondo kulia

    Sure Boy na Morris kulia

    Boban na Nyoni kulia

    Mwadini na Nditi kulia

    Bahanuz na Dida kulia

    Chuji na Mwadini kulia

          Nahodha Kaseja na Meneja, Lepold Mukebezi 'Taso'

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIM POULSEN AWATEMA KAPOMBE, DIDA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top