• HABARI MPYA

    Wednesday, August 15, 2012

    VIDEO YA SIMBA DAY KUFANYIWA EDITING LEO


    Hawa ndio waliotambulishwa Simba Day, juu walioanza kucheza na City Stars ya Nairobi, chini walioanzia benchi
     

    Na Mahmoud Zubeiry
    KATIKA Simba Day, Agosti 8, mwaka huu Simba SC ilitangaza usajili na kuonyesha jezi za wachezaji zikiwa na majina mgongoni kupitia screen kubwa la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- lakini wakati dirisha la usajili linafungwa leo saa 6:00 usiku, klabu hiyo inatarajiwa kufanyia ‘editing video ya Simba Day’.
    Katika Simba Day, ilionekana jezi ya Mbuyu Twite, Danny Mrwanda na Kanu Mbivayanga, lakini hivyo ni vipande ambavyo leo vinatolewa na kuingizwa vipande vipya kama vya picha za Paschal Ochieng kutoka AFC Leopard ya Kenya na Daniel Akuffo kutoka Hearts Of Oak ya Ghana.
    Simba imelazimika kurekebisha usajili wake dakika za mwishoni, baada ya kugundua mapungufu makubwa, yaliyotokana na ushauri mbaya wa Kamati yake dhaifu ya Ufundi, inayoongozwa na Mwenyekiti asiye na uzoefu wala ujuzi wa kuendana na hadhi ya klabu hiyo, Ibrahim Masoud ‘Maestro’.
    Katika marekebisho hayo, Simba imewatema beki Lino Masombo na kiungo Mbivayanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kuwasajili Ochieng na Akuffo. Lakini pia, Simba imemtema Mrwanda wakati habari zaidi zinasema kuna wachezaji wengine watatu, wawili kutoka Mali na mwingine mmoja kutoka Ivory Coast, miongoni mwao wanaweza kusajiliwa.
    Mapema jana, ilielezwa kiungo Mganda, Mussa Mudde angetemwa, lakini baadaye ikaelezwa huyo hataaachwa tena, badala yake wanasubiriwa wachezaji kutoka Mali na Ivory Coast waonekane, kisha walinganishwe na Ochieng kabla ya klabu kuamua imsajili nani.
    Simba ina kutwa moja tu hadi saa 6:00 usiku wa leo kuhakikisha inakamilisha usajili wake, tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu, wao wakiwa mabingwa watetezi.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIDEO YA SIMBA DAY KUFANYIWA EDITING LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top