![]() |
| Vikosi vya Simba (JUU) na Azam FC (CHINI) vilivyomenyana kwenye Robo Fainali ya Kombe la Kagame |
Na
Mahmoud Zubeiry
NYASI za Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, leo zinatarajiwa kuhimili mechi mbili kali za Nusu Fainali ya
michuano ya BankABC Sup8r, Mtibwa Sugar ya Morogoro wakianza kumenyana na
Jamhuri ya Pemba kabla ya Simba kukipiga na Azam FC.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Azam iliichapa Simba 3-0 na zitakutana tena kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
Mtibwa inapewa nafasi
kubwa ya kuitoa Jamhuri, lakini kuna hatari Azam FC wakapewa mshangao na Simba
SC leo.
Tangu mwanzo wa
mashindano haya, Simba imekuwa ikitumia kikosi chake cha vijana, Simba B, kilicho
chini ya kocha Suleiman Abdallah Matola, lakini kuna uwezekano leo, baadhi ya
wachezaji wakatolewa kwenye kambi ya Simba A mjini Arusha kuja kuongeza nguvu.
Uongozi wa Simba
unahitaji fedha kufidia makovu ya usajili na Sh. Milioni 40 ni nyingi, wakitoa
Sh. Milioni 10 kuwapa bonasi wachezaji kwa kutwaa Kombe, zinazobaki zinafidia
kabisa makovu ya usajili- hivyo haitakuwa ajabu nyota waliopo kambini Arusha
wakionekana Taifa leo.
Lakini Matola mwenyewe
alipozungumza na BIN ZUBEIRY alisema
kwamba anawaamini sana vijana wake kwamba wanaweza kuitoa Azam inayotumia nyota
wake wa Ligi Kuu wenye uzoefu.
“Yaani katika
mashindano haya siihofii timu yoyote. Na sihitaji mchezaji hata mmoja wa timu
ya kwanza ili kuitoa Azam, hawa vijana nilionao nawaahidi wapenzi wa Simba
kwamba watachukua Kombe hili,”alisema Matola.
Matola amewataka
wapenzi wa Simba SC kumiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa, Jumatano ya leo
katika Nusu Fainali hiyo, itayochezwa Saa 10:00 jioni baada ya Nusu Fainali ya
Kwanza, kati ya Mtibwa Sugar na Jamhuri ya Pemba.
Simba B ilitinga Nusu Fainali ya michuano ya
BankABC Sup8r kwa kishindo, baada ya kuifunga Zimamoto ya Zanzibar mabao 2-0
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao yake yote yakifungwa na kiungo
chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania, Christopher Edward kipindi
cha pili.
Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la
kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la
hatari.
Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba,
Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga
chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya
Zanzibar.
Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini
sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo,
kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza.
Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya
michuano hiyo, Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za
Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa
Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma
kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani
na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la
Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi
ilimpoteza mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi
nyekundu.
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Mtibwa Sugar iliichapa 5-0 Super
Falcon FC katika mchezo wa mwisho wa makundi. Mabao yake yakitiwa kimiani na
Shaaban Kisiga ‘Malone’ mawili, Dickson Daud, Mohd Mpoki na Ally Mohd ‘Gaucho’.
Katika Kundi A, Simba SC imeongoza kwa pointi zake nne,
baada ya kutoa sare moja na kushinda moja, ikifuatiwa na Zimamoto na Mtende
zinazofungana kwa pointi tatu kila moja, wakati Jamhuri inashika mkia kwa
pointi yake moja.
Kundi B, Mtibwa inaongoza kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na
Azam FC na Polisi Moro, zenye pointi tatu kila moja, wakati Falcon inashika
mkia, ikiwa haina pointi hata moja.
Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika
nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza
katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi
wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar
ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila
mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh.
Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5
kila moja.




.png)
0 comments:
Post a Comment