• HABARI MPYA

    Wednesday, August 15, 2012

    TFF IZUNGUMZE KWANZA NA MAZEMBE KABLA YA FIFA, WACHEZAJI WETU NDIO CHANZO CHA TATIZO

    Na Mahmoud Zubeiry

    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), hivi sasa lipo katika mgogoro na klabu bingwa mara nne Afrika, Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)- chanzo kikiwa na washambuliaji wawili, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu.
    TP Mazembe haikumruhusu Ulimwengu kurejea nyumbani kuichezea timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes katika mechi dhidi ya Nigeria na haikumruhusu Samatta na mwenzake huyo pia kurejea nyumbani kujiunga na timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana leo mjini Gaborone.
    Hii ni mara ya kwanza kwa Mazembe kufanya hivyo, wakati wachezaji wote hao wapo katika msimu wa pili kwenye klabu hiyo.
    Kwa sababu hiyo, TFF imesema inapeleka mashitaka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa klabu hiyo kutowaruhusu wachezaji kuchezea timu yao ya taifa, jambo ambalo kweli kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ni kosa.
    TFF wameikasirikia mno Mazembe- na hata kocha wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen ameikasirikia mno klabu hiyo. Binafsi, nimeumizwa na uamuzi huo wa Mazembe kutowaruhusu wachezaji, hasa nikizingatia Ngorongoro imetolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza mashindano ya U-20 Afrika, baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1 na Nigeria, ikianza kuchapwa 2-1 nyumbani na baadaye 2-0 ugenini.
    Naamini, kama Ulimwengu angeshiriki mechi zote mbili dhidi ya Nigeria, timu yetu ingekuwa na uhai zaidi- lakini kukosekana kwake, kumetusababisha siyo tu tumetolewa, bali tumetupwa nje ya mashindano kinyonge mno.
    Lakini kabla ya kuwahukumu Mazembe, tunapaswa kutafuta sababu juu ya kilichosababisha ghafla mabingwa hao wa zamani Afrika wakapuuza wito wa TFF kutuma wachezaji Dar es Salaam.
    Mara kadhaa nimekuwa nikiwaona makcha wa nchi jirani, ambazo wachezaji wake wanacheza hapa Tanzania wakija nchini kuwafuatilia wachezaji wao, mfano Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ wa Rwanda au Msoctland, Bobby Williamson wa Uganda.
    Wanapokuwa hapa hujionea wachezaji wao namna wanavyocheza na kufanya uteuzi kwa ajili ya timu taifa, juu ya wachezaji ambao wanawajua fika. Micho anakwenda hatua kadhaa zaidi, anawahangaikia wachezaji wa Rwanda kupata timu Ulaya, au nchi nyingine Afrika, ambako watakusanya uzoefu zaidi na baadaye kuisaidia Amavubi.
    Ulimwengu
    Lakini sijawahi kusikia hata siku moja kocha wa timu ya taifa si Kim Poulsen, tangu Mdenmark mwingine, Jan Poulsen aliyemrithi Marcio Maximo kutoka Brazil akisafiri kwenda DRC kuwafuatilia Samatta na Ulimwengu, ama Kenya ambako katika Ligi Kuu tuna mtu anaitwa Idrisa Rajab au Angola ambako tuna mtu anaitwa Said Maulid.
    Huwezi kuniambia eti leo SMG ana uzee wa kutekelezwa moja kwa moja timu ya taifa bila kuzingatia uwezo wake unaomuweka katika moja ya ligi kubwa Afrika, Girabola, wakati mwaka 2000 mchezaji huyo akisajiliwa Simba SC kutoka Kigoma, Shaaban Nditi alikuwa anacheza Singida United Ligi Kuu na akina Kipanya Malapa na Edward Rodgers Kayoza.
    Wakati fulani, Jan Poulsen alikwenda Sweden kumfuatilia Athumani Machuppa, kwa kuwa ni pua na mdomo na Denmark- lakini zaidi makocha wa Taifa Stars wamekuwa na desturi ya kusubiri sifa za wachezaji kupitia vyombo vya habari ndipo wawaite, ndio maana historia inamtaja Amy Ninje kama mmoja wa wachezaji wa zamani wa Taifa Stars.
    Baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria, Flying Eagles, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kumuita kiungo Adam Nditi wa Chelsea ya vijana ya England, ambaye tayari ameingia kwenye programu za kukomazwa kwenye kikosi cha wakubwa cha mabingwa hao wa Ulaya.
    Sijui jitihada gani za dhati zilifanyika- lakini nachokiona hapa kocha anatakiwa kusafiri hadi London na kufika Stamford Bridge kukutana na makocha wa Nditi kuzungumza nao kuhusu huyo mchezaji na kuzungumza naye mchezaji mwenyewe pia, kuliko kuzungumza kwenye vyombo vya habari.
    Samatta akikabiliana na Kolo Toure wa Ivory Coast
    TFF inapaswa kumpa fungu hata Kim akafuatilie na kujua kuhusu Nditi kama yupo kwenye nafasi ya kuchezea Tanzania, kulikoni kuamua kwa kudhani tukiwa hapa nyumbani.
    Kama sakata la Mazembe. TFF inataka kupeleka malalamiko CAF, lakini imekwishazungumza kwa kina na uongozi wa klabu hiyo ili kujua tatizo ni nini? Au inataka kutumia mabavu tu kwa sababu kanuni za FIFA zinasema klabu lazima ziwaruhusu wachezaji kuchezea timu zao za taifa?
    Nauliza hivyo, kwa sababu miezi miwili iliyopita nilifanya mahojiano na Makamu wa Rais wa Tout Puissant Mazembe, Mohamed Kamwanya ambaye alisema kwamba Ulimwengu anachelewa kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, kwa sababu kiwango chake bado kidogo.
    Alisema kwamba, Ulimwengu kila anapopewa ruhusa ya kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa, kwanza huchelewa kurudi Lubumbashi na pia hurudi akiwa hayuko fiti.
    “Hicho ndio kinamchelewesha, lakini kama siyo hivyo angekuwa anacheza tu kama mwenzake. Na nyinyi watu wa vyombo vya habari mtusaidie, kwa sababu wachezaji wakija huko wanafanya anasa, wanarudi huku hawako fiti, sasa inakuwa mbaya,”alisema Kamwanya.
    Akiwa anaingia msimu wa pili tangu asajiliwe na Mazembe, lakini Ulimwengu bado yupo kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba wa timu hiyo na hachezi Ligi Kuu wala Ligi ya Mabingwa, kama mwenzake Mbwana Ally Samatta ambaye anang’ara.
    Mimi najua kama Ulimwengu anapotoka kambini ama Ngorongoro au Taifa Stars, hubaki Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki moja au zaidi akijirusha na kuna mtu aliwahi kunisumulia ‘balaa lake’, nilikoma mwenyewe. Bado kijana mdogo, bado hajajitambua kwa sababu yeye ni Mtanzania kama wachezaji wengine waliomtangulia akina Athumani China, Edibily Lunyamila na wengineo.  
    Kuhusu Samatta, alisema huyo anaendelea vizuri na hawana tatizo naye. Lakini Samatta huyu huyu, kuna wakati Jan Poulsen alimtema timu ya taifa baada ya kutoridhishwa na kiwango chake na kipindi ambacho alimfungia vioo kilimsaidia mchezaji huyo siyo tu kujihakikishia namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Mazembe mbele ya washambuliaji hodari kama Given Singuluma na Tressor Mputu Mabi, bali pia kupandisha kiwango chake.
    Naona TFF na makocha wa timu za taifa, wana wajibu wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji. Kwa sasa wachezaji wa nje, ambao wanategemewa timu za taifa ni wawili, tu hao wa TPM- sioni ugumu wa kutengeneza mawasiliano na uongozi wa klabu hiyo, ikiwa kitaasisi kidogo tu (bongostaz.blogspot.com) kinaweza kuwasiliana na uongozi wa juu wa klabu hiyo.
    Sioni sababu ya kuingia kwenye mgogoro na Mazembe ambao wanatulelea vijana wetu vizuri na wanaendelea vizuri kwa matumaini makubwa. Naona, vema TFF ifanye mazungumzo na uongozi wa Mazembe, kutatua suala hili kuliko kufikiria kwanza kuanza kushitakiana CAF na FIFA. Nawatakia mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan katika siku hizi za ukingoni. Wasalam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF IZUNGUMZE KWANZA NA MAZEMBE KABLA YA FIFA, WACHEZAJI WETU NDIO CHANZO CHA TATIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top