 |
| Waziri Mkuu, Mh Pinda kushoto, akiwa na Mama Fatuma Karume kulia. Katikati ni Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' nje ya ukumbi wa Bunge, Dodoma leo. |
Na Mahmoud Zubeiry, Dodoma
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya Dar
es Salaam asubuhi ya leo wameonyesha Kombe lao ubingwa wa michuano hiyo,
maarufu kama Kombe la Kagame katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, mjini Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Mama Anna Makinda baada ya kumaliza kikao
cha asubuhi alianza kutambulisha wageni mbalimbali waliotembelea Bungeni leo na
ukumbi wa Bunge uliripuka kwa shangwe nzito, alipofikia kuwatambulisha mabingwa
hao wa Kagame.
Mama Anna Makinda, alianza kwa kuwatambulisha viongozi wa
Yanga, Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Mama Fatuma Karume, Francis Kifukwe na
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe
wengine kabla ya kukiinua kikosi kizima wafalme wa soka kwa nchi 12 barani Afrika.
Wakati wa zoezi hilo, Wabunge ambao ni wapenzi wa Simba, mahasimu
wa jadi, wa Yanga, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wekundu hao wa Msimbazi, Alhaj
Ismail Aden Rage, walianza kuwabeza wapinzani wao hao, kwa kuwakumbushia kipigo
cha mabao 5-0 walichowapa katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu.
Lakini hiyo haikuzuia sherehe za Yanga kuendelea hadi nje ya
ukumbi wa Bunge, ambako Wabunge na Mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda walipiga picha na wachezaji, viongozi na Kombe lao
hilo.
Wabunge wengine na Mawaziri, ambao ni wapenzi wa Simba
wakiwemo Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makala, Mbunge
wa Kinondoni, Iddi Azam na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia nao pia
walijumuika kupiga picha na Yanga.
Baada ya hapo, wachezaji wa Yanga na viongozi walikwenda
kwenye ukumbi mdogo wa Bunge kukutana na Uongozi wa Tawi la klabu hiyo, Bungeni
chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed Hamisi Misanga uliochaguliwa Julai 31, mwaka huu
ambako huko Mama Karume alizindua rasmi tawi hilo.
Yanga, waliotwaa Kombe hilo mara mbili mfululizo sasa,
wachezaji wake waliwasili usiku wa jana na baadhi ya viongozi, Wajumbe wa
Kamati ya Utendaji, Titus Osoro, Mohamed Bhinda na George Manyama pamoja na
Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa na Meneja, Hafidh Suleiman, wakati Mwenyekiti,
Yussuf Manji na Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe wengine waliwasili mapema
leo.
Kwa upande wa timu, wachezaji walifika pia jana na makocha
wasaidizi, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani Samatta, wakati kocha Mkuu,
Mbelgiji Tom Saintfiet alikuja leo pamoja na viongozi hao wakuu na Wajumbe wa
Baraza la Wadhamini, Francis Mponjoli Kifukwe na Mama Fatuma Karume.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo
wiki iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0,
ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider
Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga
inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika
fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa,
ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975
ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala,
Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba
‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja
wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga
ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
 |
| Mh Pinda akiwa kikosi cha Yanga na kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet |
 |
| Wachezaji mjengoni |
 |
| Cannavaro akionyesha Kombe kwa wabunge |
 |
| Mh Nkamia akiwa na Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa |
 |
| Mh Azzan akiinua Kombe, kulia kwake ni Mh Pinda na Martha Mlala |
 |
| Mama Karume akiwa na BIN ZUBEIRY ndani hya ukumbi mdogo wa Bunge |
 |
| Mh Makalla kulia akisalimiana na Manji. Katikati ni Mh Mtemvu |
 |
| Mh Makalla akiwa ameshika kwa pamoja Kombe na Manji. Katikati ni Cannavaro |
 |
| Mh Makalla akisalimiana na Kocha Tom |
 |
| Mh Pinda na wadau mbalimbali wa Yanga, wakiwemo Wabunge na Mawaziri |
 |
| Mh Makalla wa pili kutoka kulia akiwa na Mhariri wa Habari Leo, Eric Anthony. Kulia kwake Makalla ni Kevin Yonda na kushoto kwa Eric ni Athumani Iddi 'Chuji' na Mwigulu Lameck Mchemba, Mbunge wa Iramba Magharini |
 |
| Mh Pinda na wadau wa Yanga |
 |
| Manji akiteta na William Ngeleja |
 |
| Mh Pinda akiwa na BIN ZUBEIRY |
 |
| Wachezaji mjengoni |
 |
| Kocha Tom, Mohamed Bhinda na Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga, Bakili Makele |
0 comments:
Post a Comment