![]() |
Mtakatifu Tom kulia |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji amesema anawataka Sofapaka waliofunga Simba mabao 3-0 jana na kwa kuwa amewapa viongozi wa klabu jukumu la kumtafutia mechi moja zaidi ya kujipima nguvu na timu hiyo ya Kenya ipo Dar es salaam anaendelea kusubiri majibu.
“Nasubiri jibu kutoka kwa viongozi, ila niko tayari kucheza na timu yoyote, hata hiyo ya Kenya iliyoifunga Simba leo,”alisema Mtakatifu Tom jana.
Mapema juzi, kocha huyo alisema kwamba timu yake iko imara sasa tayari, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 15, mwaka huu, ingawa anaendelea kutafuta mechi moja zaidi ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Mtakatifu Tom alisema kwamba katika mazoezi yanayoendelea sasa, anawakosa wachezaji wanne, ambao Hamisi Kiiza aliye na timu yake ya taifa ya Uganda, Nurdin Bakari ambaye ni majeruhi, Salum Telela na Said Mohamed ambao wanaumwa Malaria.
Kocha Saintfiet anajivunia rekodi ya kushinda mechi 10 kati ya 11 alizoiongoza timu hiyo tangu ajiunge nayo miezi miwili iliyopita.
Katika mechi hizo, sita zilikuwa za michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame ambazo alishinda tano na kufungwa moja tu ya kwanza dhidi ya Atletico ya Burundi, akiiwezesha Yanga kutwaa Kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo Julai mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0 kwehye fainali, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni watupu baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1. Yanga Vs JKT Ruvu 2-0
2. Yanga Vs Atletico (Burundi) 0-2
3. Yanga Vs Waw Salam (Sudan Kusini) 7-1
4. Yanga Vs APR (Rwanda) 2-0
5. Yanga Vs Mafunzo (Z’bar) 1-1 (5-3penalti)
6. Yanga Vs APR (Rwanda) 1-0
7. Yanga Vs Azam 2-0
8. Yanga Vs African Lyon 4-0
9. Yanga Vs Rayon (Rwanda) 2-0
10. Yanga Vs Polisi (Rwanda) 2-1
11. Yanga Vs Coastal Union 2-1
0 comments:
Post a Comment