• HABARI MPYA

    Thursday, April 11, 2013

    MAJERUHI WAONGEZEKA YANGA, LAKINI YATAMBA USHINDI LAZIMA JUMAMOSI

    Majeruhi; Stefano Mwasyika

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC itamkosa beki wake Stefano Asangalwisye Mwasyika katika mchezo wa keshokutwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Mwasyika ameingia kwenye orodha ya majeruhi Yanga, akisumbuliwa na maumivu ya chini ya kisigino.
    “Habari mbaya kidogo, Mwasyika naye ni majeruhi na hatutarajii kuwa naye katika mchezo wa keshokutwa,”alisema Kizuguto.
    Kizuguto amewataja wachezaji wengine majeruhi kwa sasa Yanga SC ni beki Ladislaus Mbogo aliyefanyiwa upasuaji wa nyama za shavu, kiungo Omega Seme anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na mshambuliaji Jerry Tegete anayesumbuliwa na maumivu ya goti.
    Pamoja na hayo, Kizuguto amesema Yanga imeendelea na mazoezi yake leo katika Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na wachezaji wameonyesha ari kubwa.
    “Kwa kweli mazoezi ya leo yalikuwa mazuri mno, wachezaji wameonyesha wako vizuri sana na tunatarajia matokeo mazuri Jumamosi,”alisema.
    Aidha, Kizuguto amesistiza msimamo wa uongozi kutoruhusu mechi zao kuonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya SuperSport ya Afrika Kusini bila malipo.
    “Msimamo wa klabu ni ule ule, hatutawaruhusu SuperSport kurusha mechi yetu Live, hadi kwanza tukae chini tujadili tujue tutapata nini,”alisema Kizuguto.
    TFF, Shirikisho la Soka Tanzania lina makubaliano maalum na SuperSport kurusha baadhi ya mechi za Ligi Kuu, kwa lengo la kuitangaza ligi hiyo, lakini Yanga imegoma safari hii ikidai kampuni hiyo imekwishafanya hivyo kwa kiasi cha kutosha na sasa wanataka kulipwa. 
    Yanga wanaistaajabu SuperSport kuendelea kuonyesha bure mechi za Ligi Kuu ya Bara wakati nchini nyingine zikiwemo Kenya na Uganda wanalipia.
    Yanga imeshika kasi kwenye mbio za ubingwa, ikiwa inaongoza kwa pointi zake 49, baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 43, Kagera Sugar 37 na Simba SC ambao ni mabingwa watetezi 35. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MAJERUHI WAONGEZEKA YANGA, LAKINI YATAMBA USHINDI LAZIMA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top