MSHAMBULIAJI Lionel Messi anatarajiwa kurudi uwanjani usiku wa leo, Barcelona ikirudiana na Paris Saint-Germain katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwanasoka huyo bora wa dunia alikuwa nje kwa wiki mbili baada ya kuumia nyama za paja katika mchezo wa kwanza dhidi ya PSG mjini Paris ambao uliisha kwa sare ya 2-2, hivyo mechi ya Barca ikishinda 5-0 katika La Liga dhidi ya Real Mallorca Jumamosi.
Pamoja na hayo, klabu imethibitisha alifanya mazoezi na wenzake jana jioni pamoja na mshambuliaji mwingine Pedro na beki Adriano, ambao pia walikuwa majeruhi.
"Mchezaji mmoja ambaye yuko chini ya uangalizi wa kocha... ni Leo Messi,"imesema klabu katika tovuti yake.
Mtoto anarudi: Lionel Messi alifanya mazoezi na wenzake jana kuelekea mechi dhidi ya PSG leo
Kocha Msaidizi, Jordi Roura, anayemshikia mikoba Tito Vilanova ambaye anaendelea kupata ahueni baada ya kupatiwa tiba ya saratani, amesema Barca itasubiri hadi baada ya mazoezi ya leo kabla ya kuamua kama Messi atacheza au hatacheza.
Messi amekuwa mfungaji bora katika mashindano ya Ulaya kwa misimu minne iliyopita na msimu huu amekwishafunga mabao manane, lakini anazidiwa mabao matatu na mpinzani wake mkubwa, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ambaye jana alifunga mawili dhidi ya Galatasaray mjini Istanbul.
Dani Alves akionyesha kipaji chake mazoezini jana
Tayari: Barcelona wakijifua jana tayari kwa mtanange wa leo
Ikiwa inajivunia mabao mawili ya ugenini, Barca ina nafasi kubwa ya kuifuata Real Madrid Nusu Fainali kwa mara ya sita na kujiweka sawa katika mbio za kuwania taji la tatu ndani ya miaka mitano.
Wamecheza mechi 20 za Ligi ya Mabingwa bila kufungwa Nou Camp tangu wafungwe 2-1 na Rubin Kazan, Oktoba mwaka 2009.
Wanakuja: Zlatan Ibrahimovic (kulia) na David Beckham wana matumaini ya kuiduwaza leo Barcelona


.png)