• HABARI MPYA

    Sunday, April 14, 2013

    SIMBA NA AZAM TAIFA LEO SI YA KUSIMULIWA


    Na Mahmoud Zubeiry
    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo zinatarajiwa kuwaka moto kwa mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Simba SC na Azam FC.
    Simba SC imevuliwa rasmi ubingwa jana, kufuatia ushindi wa mabao 3-0 wa Yanga dhidi ya JKT Oljoro, ambayo imefikisha pointi 52 ambazo haziwezi kufikiwa tena na Wekundu hao wa Msimbazi.
    Lakini Wekundu hao wa Msimbazi wanapambana angalau wapate nafasi ya pili, itakayowawezesha kucheza Kombe la Shirikisho mwakani.


    Tishio: John Bocco 'Adebayor' atawakosa Simba SC leo?

    WATUHUMIWA...?

    Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu baina ya timu hizo, Azam FC ilichapwa 3-1 na baada ya hapo ikawasimamisha kipa Deo Munishi na mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa tuhuma za kuhujumu timu. Lakini wanne hao wamerejeshwa kwenye timu wiki hii, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuthibitisha hawana hatia. Wote wameingia kambini tangu Jumanne Chamazi na wamekuwa wakifanya mazoezi na wenzao, je leo watacheza?
    Azam bado inawania ubingwa, ikiwa na pointi 46 nyuma ya Yanga na leo itahitaji kushinda ili kuongeza kasi yake ya kuwafukuza vinara hao wa Ligi Kuu.
    Kwa kuwa Yanga wanaamini Azam inawachelewesha kufurahia ubingwa, leo haitakuwa ajabu mashabiki wake wakiwashangilia wapinzani wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa.
    Japokuwa wengi wanaamini Simba SC imepoteza makali, kutokana na kuandamwa na mgogoro na mvurugiko ndani ya timu, lakini ukweli ni kwamba, Wekundu wa Msimbazi bado wana kikosi imara.
    Ikiundwa na mseto wa vijana waliopandishwa kutoka timu B na wachache waliokuwa kikosi cha kwanza, Simba SC inatarajiwa kutoa upinzani mkubwa kwa Azam leo na kwa ujumla mchezo utakuwa mtamu.
    Felix Sunzu na Mrisho Ngassa wataongoza safu ya ushambuliaji wakati Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba wataongoza safu ya kiungo, huku mlinda mlango Juma Kaseja akipewa nafasi kubwa ya kuanza leo chini ya ulinzi wa Shomary Kapombe, Miraj Adam, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Hassan Hatibu.
    Said Ndemla, Haroun Chanongo ni chipukizi ambao wanaweza kuanza leo, wakati Edward Christopher, Ramadhani Singano na Rashid Ismail hata wakianzia benchi, miongoni mwao wanaweza kuingia uwanjani baadaye.
    Azam FC iko sawa nayo na imeshika kasi. Katika mchezo wake uliopita wa Ligi Kuu Alhamisi ikiifunga African Lyon 3-1, kocha Muingereza Stewart Hall aliwapumzisha wachezaji wake watano wa kikosi cha kwanza.



    Mbaya wao: Mrisho Ngassa ataiadhibu timu yake ya zamani, Azam FC leo?

    Hao ni kipa Mwadini Ally, beki David Mwantika, viungo Kipre Balou, Humphrey Mieno ambaye aliingia dakika 20 za mwisho na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’, ambao wote wanatarajiwa kuanza leo.
    Bado haieleweki Stewart atapangaje safu yake ya ulinzi leo, haswa baada ya kurejea kwa kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey waliokuwa wamesimamishwa tangu Novemba mwaka jana. 
    Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, Joackins Atudo na David Mwantika- huo ndiyo ukuta wa Azam unaofahamika kwa sasa, lakini baada ya kurejea kwa wachezaji hao wanne, Stewart ataamua. 


    Mara ya mwisho Mapinduzi: Zilipokutana mara ya mwisho katika Nusu ya Kombe la Mapinduzi, Simba ilitolewa kwa penalti baada ya sare ya 2-2

    Lakini bado yupo kinara wa mabao Ligi Kuu, Kipre Herman Tchetche mwenye mabao 15 hivi sasa, ambaye bila shaka hata walinzi wa Simba wamekuwa wakimuota.
    Kipre mwenye kasi, ambaye anashambulia kutokea pembeni na pamoja kufunga mabao mazuri na ya kusisimua kwenye Ligi Kuu, lakini pia amekuwa mpishi mzuri. 
    Yupo mchezaji mwingine hatari, tena mwenye bahati ya kuifunga Simba SC, Khamis Mcha ‘Vialli’ na zaidi ni safu imara ya kiungo chini ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’- pata picha ni burudani kiasi gani ipo Taifa leo.
    Kwa upande mwingine, mechi ya leo itakuwa muhimu sana kwa kocha Mfaransa, Patrick Liewig juu ya mustakabali wake kwenye timu baada ya yote aliyoyafanya tangu aanze kazi Januari ambayo yamebadilisha kabisa taswira ya kikosi cha kwanza cha Simba SC.  
    Kocha huyo wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa na klabu ya ASEC Mimosa ya Ivory Coast, amewaengua kwenye programu yake wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza akina Paul Ngalema, Amir Maftah, Juma Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban’, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Abdallah Juma na kuamua kutumia yosso zaidi.
    Kama ataipa ushindi Simba SC leo na timu aliyonayo sasa, wazi atajihakikishia kuendelea na kazi Msimbazi hadi msimu ujao na hasa timu ikicheza kandanda ya kuvutia na tofauti ya hapo haitakuwa ajabu hata hii ikiwa mechi yake ya mwisho katika klabu hiyo. 
    Katika mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa; Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Hassan Hatibu, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher na Mrisho Ngassa.
    Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’, Salum Abubakar, John Bocco, Humphrey Mieno na Kipre Tchetche.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA NA AZAM TAIFA LEO SI YA KUSIMULIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top