• HABARI MPYA

    Friday, April 12, 2013

    TFF YASEMA PRIMO ATAKUWA NCHINI JUMATATU KUTATUA MGOGORO WA UCHAGUZI


    Ndite huyu; Primo Corvaro
    Na Michael Wambura
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kwamba ujumbe wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) utawasili nchini Jumatatu (Aprili 15 mwaka huu) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF.
    Kwa mujibu wa taarifa kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo Corvaro na utafanya kazi kwa siku tatu kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili 18 mwaka huu.
    Ukiwa nchini, ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.
    Wajumbe hao wangependa kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF imeiandikia Wizara ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na wakuu wengine wa michezo Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi zao.
    Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni Jamal Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.
    Wengine ni Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata rufani FIFA.
    Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.
    Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa upya, kukataliwa.
    Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.
    Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.
    "Shirikisho linawaomba wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya kutosha na kwamba barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa),:"imesema taarifa ya TFF.
    Mapema wiki hiii, BIN ZUBEIRY ilikuwa chombo cha kwanza cha habari nchini kuandika juu ya Primo kuongoza msafara wa FIFA kuja nchini kutatua mgogoro wa uchaguzi wa TFF. 

    PROGRAMU YA UJUMBE WA FIFA NCHINI
    Tarehe /Muda

    Tukio
    15 Aprili 2013
    Saa 12:30 – 03:00
    Kuwasili kwa wajumbe wa FIFA
    15 Aprili 2013
    Saa 04:00 – saa 05:00 usiku
    Kikao na Rais wa TFF pamoja na Sekretarieti
    16 Aprili 2013
    Saa 04:00 – 05:00 asubuhi
    Kwenda ofisini kwa Waziri wa Michezo kwa ajili ya kumsalimu
    16 Aprili 2013
    Saa 05:30 – 06:30 asubuhi
    Kukutana na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kupata taarifa ya uchaguzi
    16 Aprili 2013
    Saa 06:30 – 08:00 mchana
    Chakula cha Mchana
    16 Aprili 2013
    Saa 08:00 – 12:00 jioni
    Kukutana na wagombea walioondolewa
    17Aprili 2013
    Saa 03:00 – 05:00 asubuhi
    Kukutana na Kamati ya Rufa za Uchaguzi ya TFF
    17 Aprili 2013
    Saa 05:30 – 06:30
    Mchana
    Kupewa taarifa zinazohusiana na mchakato wa uchaguzi, i.e., kesi zilizo mahakamani

    17 Aprili 2013
    Saa 08:00 – 10:00 jioni
    Kukutana na watu wengine ambao FIFA wanaweza kuomba kukutana nao
    17Aprili 2013
    Saa 10:30 – 11:00 jioni
    Mkutano na waandishi wa habari – kushukuru mamlaka na pande zilizohusika kwa ushirikiano
    18 Aprili 2013
    Saa 10:00 – 12:00 Alfajiri
    Kuondoka hotelini kwa ajili ya safari

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TFF YASEMA PRIMO ATAKUWA NCHINI JUMATATU KUTATUA MGOGORO WA UCHAGUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top