![]() |
Simba SC kazini kesho |
Na Boniface Wambura, MEI 7, 2013
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea kesho kwa timu za Simba na Mgambo Shooting ya Tanga kuumana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 20,000.
Simba SC inahitaji kushinda mechi hiyo ili kuimarisha mbio zake za kuifukuza Azam FC katika nafasi ya pili.
Mabingwa hao wa msimu uliopita, kwa sasa wana pointi 42 na wanaiombea duwa mbaya Azam, ipoteze mechi zake mbili zilizobaki na wao washinde mechi zao mbili dhidi ya Mgambo kesho na Yanga SC Mei 18, wawe wa pili.
Simba SC inaweza kufikisha pointi 48, ambazo tayari Azam FC inazo. Ikiwa Azam itapoteza mechi mbili zilizobaki na Simba ikashinda zote, mshindi wa pili ataamuliwa kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Ikumbukwe, mshindi wa pili wa Ligi Kuu hucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na bingwa ambaye tayari amepatikana, Yanga SC watacheza Ligi ya Mabingwa.
Wakati huo huo; Mechi namba 111 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Simba iliyochezwa juzi (Mei 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kushinda mabao 3-1 imeingiza sh. 17,700,000.
Watazamaji 3,163 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,485,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,700,000.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 2,901 na kuingiza sh. 14,505,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 28 na kuingiza sh. 560,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,772,416.50, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,063,449.90, Kamati ya Ligi sh. 1,063,449.90, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 531,724.95, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 206,781.93 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 206,781.93.