• HABARI MPYA

    Tuesday, July 09, 2013

    TENGA APIGA MADONGO USAJILI SIMBA NA YANGA

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA JULAI 9, 2013 SAA 1:00 USIKU 
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema katika kipindi hiki cha usajili vema klabu ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
    Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9 mwaka huu), Tenga amesema tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa kuhimili dakika 90.
    Tenga amesema kwa sababu hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi ambayo timu zao zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya wachezaji wanaotaka kusajiliwa.
    Amerudi Yanga SC; Mrisho Ngassa amesajiliwa Yanga SC kutoka Simba SC, usajili wake wa kitaalamu?

    Kauli ya Tenga ni kama anazipiga madongo klabu kongwe nchini Simba na Yanga ambazo wazi viongozi ndio hufanya usajili kwa utashi wao na si makocha.
    Pamoja na hayo, Tenga amezungumzia mchakato wa marekebisho ya Katiba na kusema hakuka hila yoyote kama watu wanavyodhani, kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Rais Tenga amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila mtu apate haki yake.
    Amesema Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili katika Katiba ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye uanze mchakato wa uchaguzi.
    “Katika kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia ile ile ya FIFA, tusitengeneze kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,” amesema.
    Rais Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo wanatakiwa kuyatekeleza ili wasonge mbele.
    “Tutawaeleza kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu kimoja), ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja wanasikilizwa. Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza utatolewa muda wa kutosha wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.
    Wakati huo huo: TFF imevitaka vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwasilisha ratiba zao za michuano ya U15 Copa Coca-Cola kabla ya Julai 15 mwaka huu.
    Ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa 16 pekee ambavyo ndivyo vimewasilisha TFF ratiba hizo mpaka sasa. Jumla ya mikoa 32 ya Tanzania Bara na Zanzibar inashiriki katika michuano hiyo ya umri chini ya miaka 15 kuanzia ngazi ya wilaya ambapo ngazi ya mikoa inatakiwa kuanza Julai 15 mwaka huu.
    Mikoa ambayo tayari imewasilisha ratiba zao ni Arusha, Ilala, Kagera, Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kigoma, Kinondoni, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Mara, Mjini Magharibi, Morogoro, Singida, Tanga na Temeke.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TENGA APIGA MADONGO USAJILI SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top