• HABARI MPYA

    Wednesday, November 05, 2014

    HIZO NDIZO ADHA ZA KUBADILISHA MAKOCHA KAMA ‘SHATI’, TAMBWE NA KIIZA WA KAZI GANI SASA!

    JAMBO moja wasilopenda wachezaji duniani kote, ni kubadilishiwa makocha mara kwa mara. Unajua kwa sababu gani?
    Mchezaji anapokuwa katika timu, wakati wote hachezi kwa mawazo yake, bali anafuata mawazo ya kocha. Sasa kuwabadilishia walimu mara kwa mara, kunawapa mzigo wachezaji wa kushika mawazo ya mbinu za falsafa mpya za ufundishaji wa mwalimu mpya.
    Falsafa yoyote ya ufundishaji ya mwalimu, inahitaji na aina ya wachezaji ambao ataamini wataweza kuendana nayo.
    Kwa hivyo, ndiyo maana mwalimu mpya anapoingia kwenye timu, lazima utaona mabadiliko- baadhi ya wachezaji waliokuwa hawapati nafasi chini ya mwalimu aliyetangulia, wataanza kupangwa.

    Si ajabu, wachezaji waliokuwa tegemeo wataonekana hawafai na kutupwa nje ya kikosi cha kwanza. Imekwishatokea sana tu.
    Jose Mourinho aliingia Cheslea na kumkuta Msenegali, Demba B akiwa tegemeo la mabao The Blues, lakini Mreno huyo akamuondoa taratibu hadi kumuuza kabisa msimu huu.
    Eti Demba Ba alikuwa anawekwa benchi na ‘babu’ Samuel Eto’o msimu uliopita na msimu huu kauzwa, amerejeshwa ‘kikongwe’ mwingine, Didier Drogba. Hao ndiyo makocha.
    Yanga SC ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita nyuma ya Azam FC.
    Mchezaji Mganda, Hamisi Kiiza ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa timu msimu huo na wa tatu katika wafungaji bora wa Ligi Kuu, nyuma ya Mrundi Amisi Tambwe wa Simba na Kipre Tchetche wa Azam, raia wa Ivory Coast.
    Msimu uliopita, Yanga SC ilipitia mikononi mwa makocha wawili wa Kiholanzi, kwanza Ernie Brandts na baadaye, Hans van der Pluijm ambao walimpa nafasi Kiiza katika kikosi cha kwanza.
    Lakini msimu huu, Yanga SC ina kocha Mbrazil, Marcio Maximo na Kiiza hayumo kwenye kikosi cha kwanza na badala yake, Mbrazil mwenzake kocha huyo, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ ndiye amechukua nafasi.
    Kiiza amekuwa akipewa nafasi mara chache na Maximo, tena akitokea benchi- hajawahi kuanzishwa hata mara moja chini ya Mbrazil huyo.
    Mfumo pia wa uchezaji umebadilika na sasa mkali mwingine wa mabao wa timu hiyo msimu uliopita, Mrisho Ngassa hatakiwi kufunga, bali kumsetia Jaja, ambaye kasi yake ya ufungaji hairidhishi hadi sasa.
    Simba SC nao msimu uliopita walikuwa chini ya Mcroatia, Zdravko Logarusic aliyempokea mzalendo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’.
    Tambwe alikuwa chaguo la kwanza mbele ya walimu wote hao katika msimu wake wa kwanza Simba SC na mwisho wa msimu akawa mfungaji bora.
    Lakini baada ya ujio wa kocha mpya, Mzambia Patrick Phiri msimu huu, Tambwe amepoteza nafasi kikosi cha kwanza. Tena, Phiri alitaka Tambwe aachwe katika usajili, lakini uongozi ukapinga.
    Kweli, mustakabali wa Tambwe si mzuri kwa sasa kwenye kikosi cha Simba kwa sababu amekwishanukuliwa mara kadhaa akisema anaomba aruhusiwe kuondoka kwenda kwenye timu ambayo atakuwa anacheza.
    Si mchezaji mbaya, anajua kufunga, lakini aina ya uchezaji wa Tambwe haiingii kwenye mipango ya Phiri, sasa wa kazi gani katika timu.
    Vivyo hivyo kwa Kiiza, Diego wa Kampala ni mfungaji hodari, lakini uchezaji wake haumvutii kocha Maximo- sasa wa nini katika timu?
    Hizo ndizo adha za kubadilisha makocha kama ‘shati’. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIZO NDIZO ADHA ZA KUBADILISHA MAKOCHA KAMA ‘SHATI’, TAMBWE NA KIIZA WA KAZI GANI SASA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top