• HABARI MPYA

    Tuesday, November 04, 2014

    MANYIKA MDOGO ASEMA IVO ANAMPA ‘TAFU’ SANA SIMBA SC

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KIPA wa tatu wa Simba SC, Peter Manyika amesema anamshukuru kipa wa kwanza wa klabu hiyo, Ivo Mapunda kwa ushirikiano mkubwa anaompa katika wakati huu mgumu.
    Manyika amelazimika kupewa dhamana ya kulinda lango la Simba SC kuanzia mwezi uliopita baada ya makipa wote Ivo na wa pili, Hussein Sharrif ‘Casillas’ kuwa majeruhi.
    Na kipa huyo mwenye umri wa miaka 19 amesema kwamba Ivo amekuwa akimjenga kisaikolojia wakati wote, kabla na baada ya mechi ili aweze kufanya kazi kwa kujiamini.
    “Kudakia timu kubwa kama Simba si jambo rahisi. Nadhani imeshuhudiwa wanasajiliwa makipa ambao wametoka klabu za Ligi Kuu wakifanya vizuri, lakini wakifika hapa wanashindwa,”.
    Peter Manyika amemshukuru Ivo Mapunda kwa msaada mkubwa anaompa hivi sasa

    “Pia wanasajiliwa makipa hadi wa timu za taifa za nje, lakini wakifika hapa wanashindwa. Simba ni klabu kubwa, ambayo inabidi uwe na moyo wa ujasiri kufanya kazi. Sasa hiyo ndiyo kazi ambayo kaka Ivo anaifanya kwangu,”amesema.
    Mtoto huyo wa kipa namba moja wa Taifa Stars na klabu za Sigara, Yanga SC na Mtibwa Sugar amesema kwa kweli hatamsahau daima Ivo katika maisha yake.
    “Wakati nasaini Simba, nilijua siku moja nitadaka, lakini sikutegemea kama itakuwa mapema kiasi hiki. Na ilipotokea dharula hiyo, baba (Manyika Peter) aliniambia fanya kazi, unaweza. Bahati nzuri katika timu nako napewa sapoti na kila mtu, hadi viongozi, makocha na wachezaji wenzangu,”amesema.
    Ameongeza kwamba anafurahi zaidi kuona hata mashabiki wa timu Dar es Salaam na mikoani wanampa sapoti kubwa, jambo ambalo linazidi kumjengea hali ya kujiamini.
    Manyika mdogo ameshukuru vyombo vya habari pia kwa kumjenga kisaikolojia na amesema kwamba atajitahidi kuongeza bidii ya mazoezi, kujifunza na ubunifu ili kumfurahisha kila mmoja anayemuunga mkono wakati huu.
    Amekiri kuna makosa madogo madogo ambayo anayafanya wakati huu, ambayo mengi yanatokana na kwamba ndiyo anaanza kudaka Ligi Kuu, lakini amesema amekuwa akijifunza kila siku.
    “Najifunza kila siku, kwa mimi mwenyewe kujiuliza baada ya mechi, watu kunishauri na kikubwa zaidi ni baba na Ivo. Baba kila mechi nayocheza anatazama kwenye Televisheni na ikiisha ananiambia, hapa hivi, pale hivi, fanya hivi,”anasema.
    Hadi sasa, kipa huyo ameidakia mechi tatu za mashindanio Simba SC akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili, mara moja katika kila mechi mbili za mikoani kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Prisons mjini Mbeya na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
    Alidaka kwa umahiri dhidi ya mahasimu Yanga SC, Oktoba 18, mwaka huu timu hizo zikitoka sare ya bila kufungana kabla ya kupangua mkwaju wa penalti wa David Luhende katika mechi na vinara wa Ligi Kuu, Mtibwa Sugar.      
    Awali ya hapo, alidaka mechi tatu za kirafiki Afrika Kusini, ya kwanza akiingia dakika ya 43 baada ya Casillas kuumia na akamalizia bila kufugwa dhidi ya Orlando Pirates, wakati mechi zilizofuata alifungwa jumla ya mabao sita, Simba ikichapwa 4-2 na Bidvest Wits na 2-0 na Jomo Cosmos.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANYIKA MDOGO ASEMA IVO ANAMPA ‘TAFU’ SANA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top