TANZANIA jana ilianza vibaya michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya kufungwa bao 1-0 na Madagascar Uwanja wa Free State Toyota.
Bao lililoizamisha Taifa Stars lilifungwa na mshambuliaji Toky Rakotondraibe Niaina dakika ya 28 akimtungua kipa Yakoub Suleiman Ali.
Taifa Stars itacheza mechi yake ya pili na ya mwisho ya Kundi C dhidi ya Eswatini Jumatano ikihitaji lazima ushindi ili kwenda Nusu Fainali.
Kesho Madagascar watarudi Uwanja wa Toyota Free State kukamilisha mechi zake za Kundi C kwa kumenyana na Eswatini.
Mchezo wa jana dhahiri Taifa Stars iliathiriwa na uchovu baada ya kusafiri usiku kucha wa kuamkia jana ikitokea Polokwake ambako iliondoka Saa 6:00 usiku juzi na kufika Bloemfontein Saa 1:00 asubuhi ya jana.
Hiyo ni baada ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya wenyeji, Bafana Bafana uliomalizika kwa sare ya bila mabao usiku wa juzi Uwanja wa Peter Mokaba Jijini Polokwane, zamani Pietersburg.
Lakini pia Taifa Stars iliwakosa wachezaji tisa kati ya waliocheza mechi ya jana na Bafana Bafana akiwemo kiungo mshambuliaji wa Wydad Athletic ya Morocco, Suleiman Mwalimu Abdallah ‘Gomez’.
Pamoja na kocha Hemed Suleima Ali ‘Morocco’ kumpanga aanze jana, lakini chipukizi huyo aliumia jicho wakati wa mazoezi ya awali kabla ya mchezo baada ya kugongana na mwenzake akiwa anapiga kichwa.
Wengine wanane waliondokea Polokwane kwenda kujiunga na klabu zao kwa ajili ya mechi za kumalizia msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Hao ni kipa Ally Salim, mabeki Mohamed Hussein na Abdulrazak Hamza, kiungo Yusuph Kagoma na washambuliaji Kibu Dennis na Valentino Mashaka wote wa Simba na mabeki, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na Dickson Job wote wa Yanga.
0 comments:
Post a Comment