Kikosi cha Taifa Stars kiliwasili Uwanja wa Ndege wa OR Tambo Jijini Johannesburg Saa 2:00 kwa saa za Afrika Kusini, saa moja zaidi kwa saa za nyumbani bila wachezaji wawili, beki Shomari Kapombe wa Simba ambaye ni mgonjwa na winga, Suleiman Mwalimu ‘Gomez’ wa Wydad Athletic ya Morocco ambaye atawasili baadaye kesho.
Nahodha wa Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema nia yao ni kupata matokeo mazuri dhidi ya Bafana Bafana Ijumaa na kwa ubora wa kikosi chao wanaamini hilo litawezekana.
Baada ya mchezo wa kirafiki na Bafana Bafana Ijumaa, mapema Jumamosi Taifa Stars itasafiri kwenda mjini Bloemfontein kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) inayotarajiwa kuanza kesho, Juni 4 Uwanja wa Free State Toyota.
Adha, Mkuu wa Msafara wa Taifa Stars, James Mhagama amesema kwamba wamekuja hapa kuendeleza rekodi yao nzuri kwenye michuano ya COSAFA, hivyo hawawahofii wapinzani wao wa Kundi C, Madagascar na Eswatini.
Kwenye Kombe la COSAFA Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Ewatini na Madagascar, wakati Kundi A wapo wenyeji Afrika Kusini, Mauritius, Msumbiji na Zimbabwe na Kundi B linazikutanisha Angola, Lesotho, Malawi na Namibia.
Taifa Stars itacheza mechi yake ya kwanza ya COSAFA Juni 7 dhidi ya Madagascar kabla ya kumalizia na Eswatini Juni 11 kuangalia mustakabali wake wa kwenda Nusu Fanali ambazo zitafuatia Juni 13 na Fainali ni Juni 15 sambamba na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Mara ya mwisho Tanzania ilishiriki michuano ya COSAFA mwaka 2017 Jijini Rusternburg nchini Afrika Kusini na kutolewa katika hatua ya Nusu Fainali ikifungwa mabao 4-2 na Zambia Julai 5, mabao ya Taifa Stars yakifungwa na Erasto Nyoni dakika ya 16 na Simon Msuva dakika ya 85, huku ya Chipolopolo yakifungwa na Brian Mwila dakika ya 44, Justin Shonga mawili dakika ya 45+2′ na 68 na Jackson Chirwa kwa Penalti dakika ya 56.
Taifa Stars ilianza vyema kwa kuongoza Kundi A mbele ya Angola, Mauritius na Malawi ikivuna ponti tano na kuizidi tu wastani wa mabao Angola, huku Mauritiusn na Malawi kila moja ikiambulia pointi mbili.
Taifa Stars ambayo mechi zake za Kundi A iliifunga Malawi 2-0 na kutoa sare ya 0-0 na Angola na 1-1 na Mauritius – kwenye Robo Fanali iliwatoa wenyeji, Bafana Bafana bao pekee la mshambuliaji Elias Maguri dakika ya 18.
0 comments:
Post a Comment