RASMI leo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limetangaza kummwaga kocha Jan Borge Poulsen katika timu ya taifa, Taifa Stars
na kumpa mikoba yake, Kim Poulsen (pichani kushoto) aliyekuwa kocha wa timu za vijana kuanzia leo,
Mei 11 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema Kim amepewa mkataba wa mwaka
mmoja baada ya Shirikisho kuamua kutomuongezea mkataba Jan. Mkataba wa Jan
uliokuwa wa miaka miwili unamalizika Julai 30 mwaka huu.
Amesema kwa vile Taifa Stars inakabiliwa na
mechi za mchujo za Kombe la Dunia raundi ya pili Kanda ya Afrika na mechi za
mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), TFF imeona ni lazima iwe na kocha
mpya mapema kabla ya mkataba wa Jan kumalizika.
Kim ambaye ni raia wa Denmark amekuwa
nchini kwa mwaka mmoja sasa akifundisha timu za Taifa za vijana wenye umri
chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na miaka 20 (Ngorongoro Heroes), hivyo
anawafahamu vizuri wa wachezaji wa Tanzania.
TFF imeanza mchakato wa kutafuta kocha
mwingine wa timu za vijana atakayeziba nafasi ya Kim. Ili kuwa na makocha wenye
falsafa moja, kocha huyo anatafutwa kutoka Denmark.
Naye Kim ambaye Jumatatu (Mei 14 mwaka huu)
atatangaza kikosi cha Taifa Stars ambacho Juni 2 mwaka huu kuivaa Ivory Coast
katika mechi ya mashindano amesema yuko tayari kwa kazi hiyo na kusisitiza
kuwepo ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili timu hiyo iweze kufanya
vizuri.
0 comments:
Post a Comment