![]() |
Nyota wa Twiga Stars, Sofia Mwasikili |
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya
Tanzania, Twiga Stars kesho inatarajiwa kumenyana na Zimbabwe katika mechi ya
kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars ambayo ilikuwa katika ziara ya
mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza imerejea leo (Mei 11 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam tayari kuikabili Zimbabwe. Ikiwa Mwanza jana ilicheza
mechi ya kirafiki dhidi Rock City Queens, lakini mechi hiyo ilivunjika dakika
ya 58 kutokana na mvua kubwa. Hadi mechi inavunjika, Twiga Stars ilikuwa
ikiongoza kwa mabao 5-0.
Kwa mujibu wa kocha wa Twiga Stars, Charles
Boniface Mkwasa, mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi
ya mashindano ya Afrika (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Mei 26
mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya kurudiana Dar es Salaam wiki mbili
baadaye.
Naye Kocha wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza
amesema amefurahi kupata mechi hiyo kwa vile anaamini Twiga Stars ni kipimo
kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya AWC dhidi ya Nigeria.
Twiga Stars na Zimbabwe zilishakutana mara
mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo
katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa
penalti 4-2.
Mechi ya pili ilikuwa michezo ya All Africa
Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka sare ya
mabao 2-2.
Viingilio katika mechi hiyo
itakayochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba kuanzia saa 10.30 jioni
ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B
ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.
0 comments:
Post a Comment