• HABARI MPYA

    Thursday, November 01, 2012

    BRANDTS: WACHEZAJI YANGA SASA WANANIKOSHA

    Brandts

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA Mhoalanzi wa Yanga, Ernie Brandts amesema kwamba taratibu wachezaji wa klabu hiyo wanaanza kushika mafundisho yake na anaamini kama wataendelea hivyo, hadi kufika Januari timu hiyo itakuwa inacheza anavyotaka.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Brandts alisema kwamba wana Yanga bado wanahitaji kuwa na subira ili kumpa fursa ya kuijenga timu vyema.
    “Si kazi ya wiki moja au mwezi mmoja, unahitajika muda ili kocha aweze kutengeneza timu ya ushindi na kucheza soka nzuri. Nahitaji muda kuwajua zaidi wachezaji na kujua namna ya kuwabadilisha, unaweza kuona taratibu timu inaanza kucheza soka ya kuvutia,”alisema.
    Brandts aliiongoza Yanga SC kuendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa Mgambo JKT ya Handeni, Tanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Yanga sasa iwe na pointi sawa na mabingwa watetezi, Simba SC waliotoa sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro leo, ingawa inazidiwa bao moja tu katika wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
    Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Didier Kavumbangu.
    Cannavaro alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Oscar Joshua dakika ya pili kutoka wingi ya kulia, wakati Kavumbangu alimalizia pasi ya Hamisi Kiiza dakika ya 39.
    Pamoja na kutoka uwanjani wamelowa kipindi cha kwanza, lakini Mgambo JKT walicheza soka ya kuvutia na mara mbili walikaribia kufunga kupitia kwa Juma Mwinyimvua.
    Yanga walicheza vema dakika 45 za kipindi cha kwanza, tofauti sana na mechi za awali ambazo wamekuwa ‘wakichezewa’ sana na wapinzani.
    Ilishuhudiwa katika kipindi hicho, Yanga wakimiliki zaidi mpira na kupeana pasi za uhakika, ingawa mashambulizi yao mengi walipitisha pembeni, hasa upande wa kulia.
    Hamisi Kiiza, Msuva na Kavumbangu walicheza kwa uelewano mkubwa pale mbele na kulitia misukosuko haswa lango la Mgambo. 
    Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto wao tena na kuendelea kuwachachafya Mgambo.
    Hata hivyo, iliwachukua Yanga dakika 34 kupata bao la tatu, mfungaji akiwa ni Jerry Tegete aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya Kavumbangu.
    Tegete alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya beki wa kushoto, Oscar Joshua.
    Pamoja na kufungwa, Mgambo waliendelea kusukuma mashambulizi langoni mwa Yanga, ingawa leo mabeki wa timu hiyo, inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts walicheza kwa uelewano mkubwa na kudhibiti hatari zote langoni mwao. 
    Mgambo inayofundishwa na Mohamed Kampira, ilipata pigo dakika ya 85, baada ya beki wake wa kulia, Salum Mlima kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea rafu mbaya Mbuyu Twite.
    Baada ya mchezo huo, Brandts alisema dakika 10 za mwanzo timu yake ilikuwa inashindwa kumalizia vizuri mashambulizi yake, lakini baadaye ikatulia na hatimaye kupata ushindi huo, ambao ameufurahia kwani unamuweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
    Kwa upande wake, Kampira wa Mgambo alisema kufungwa ni sehemu ya mchezo, akawasifu Yanga kwa kutumia nafasi walizopata, huku akijutia nafasi walizopoteza wachezaji wake leo.
    Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Nsajigwa Shadrack/Kevin Yondan dk 46, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo/Nurdin Bakari dk 76, Didier Kavumbangu/Jerry Tegete dk68, Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.
    Mgambo JKT; Godson Mmasa, Salum Mlima, Yassin Awadh, Salum Kipanga/Godfrey Komba dk80, Bakari Mtama, Ramadhani Malima, Chande Magoja, Mussa Ngunda, Issa Kandulu/Nassor Gumbo dk 60, Fully Maganga na Juma Mwinyimvua/Omar Matwiko dk76.
    Katika mchezo wa utangulizi, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Yanga, imeifunga Mgambo JKT ya vijana pia 1-0, bao hilo pekee la Clever Charles dakika ya 65.
    Katika mechi nyingine, Simba ilitoka sare ya 1-1 Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji wakitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Mokili Rambo kabla ya Amri Kiemba kusawazisha dakika ya 57. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BRANDTS: WACHEZAJI YANGA SASA WANANIKOSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top