• HABARI MPYA

    Wednesday, November 14, 2012

    TAIFA STARS YAIVAA HARAMBEE KIRUMBA KATIKA MZANI WA FIFA LEO

    Taifa Stars

    Na Mahmoud Zubeiry
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kumenyana na Kenya, Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki, ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Tanzania inakutana na Kenya, zikiwa hazitofautiani sana kwa sasa, japokuwa Harambee inajivunia wachezaji kadhaa wanaocheza soka ya ushindani Ulaya.
    Taifa Stars, inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, aliyeanza kazi Mei mwaka huu, akirithi mikoba ya Jan Borge Poulsen kutoka Denmark pia, haijashinda mechi yeyote tangu iifunge Gambia 2-1 Juni 10, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 Brazil.
    Chini ya Kim, aliyepandishwa kutoka timu za vijana za Tanzania, kazi aliyoanza Aprili mwaka jana, ilitoka sare ya 1-1 Juni 17, ilitolewa na Msumbji kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
    Ilijitupa uwanjani mara ya mwisho, katika mchezo wa kirafiki, Agosti 15, mwaka huu mjini Gaborone na kulazimishwa sare ya kufungana mabao 3-3, tena ikitoka nyuma na kusawazisha.
    Kenya inayofundishwa na Mfaransa Henri Michel, mara ya mwisho kushinda mechi ilikuwa ni Julai 12, mwaka huu ilipoichapa Botswana nyumbani kwake, Gaborone, mabao 3-1, lakini Harambee Stars katika mechi yao ya mwisho waliyocheza, walifungwa 2-1 nyumbani na Afrika Kusini Oktoba 16, mwaka huu, huo ukiwa mchezo wa kirafiki.
    Mchezo huo, unatarajiwa kuinufaisha zaidi timu ya Bara, Kilimanjaro Stars, yenye wachezaji wengi kwenye kikosi hicho, kwani baada ya hapo itaingia kambini kujiandaa na michuano ya Tusker Challenge 2012, itakayofanyika mjini Kampala, Uganda mwishoni mwa mwezi huu. Kenya pia itashiriki michuano hiyo ya Challenge.
    Wakati Kenya iliwasili Mwanza jana, Tanzania walianza kujikusanya kambini Jumapili na hadi kufikia juzi kikosi kilikuwa kimekwishakamilika.
    Wachezaji walioitwa kwa ajili ya mechi hiyo ni makipa Juma Kaseja (Simba SC) na Deogratius Mushi ‘Dida’ wa Azam FC.
    Mabeki; Kevin Yondan (Yanga), Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam FC), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na Amir Maftah (Simba).
    Viungo; Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo (Yanga) na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar).
    Washambuliaji; John Bocco ‘Adebayor’ (Azam FC), Simon Msuva (Yanga), Christopher Edward (Simba), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa (TPM, DRC).

    REKODI YA STARS MWAKA HUU NA RATIBA YA MECHI ZIJAZO:
    Februari 23, 2012
    Tanzania 0 – 0 DRC (Kirafiki)
    Februari 29, 2012
    Tanzania 1 – 1 Msumbiji   (Kufuzu Mataifa ya Afrika)
    Mei 26, 2012
    Tanzania 0 – 0 Malawi
    Juni 2, 2012
    Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 10, 2012
    Tanzania 2 – 1 Gambia      (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 17, 2012
    Msumbiji 1 – 1 Tanzania   (Tanzania ilitolewa kwa penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
    Agosti 15, 2012
    Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
    Novemba 14, 2012
    Tanzania Vs Kenya (Kirafiki)
    Machi 22, 2013
    Tanzania Vs Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 7, 2013
    Morocco Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 14, 2013    
    Tanzania Vs Ivory Coast    (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Septemba 6, 2013
    Gambia    Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TAIFA STARS YAIVAA HARAMBEE KIRUMBA KATIKA MZANI WA FIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top