• HABARI MPYA

    Thursday, April 12, 2012

    NIZAR AIBUKIA SOUTH STARS



    Nizar enzi zake Marekani
    BONANZA la Southern Zone All Stars linalotarajiwa kufanyika Mei mwaka huu na kushirikisha nyota mbalimbali wa soka na muziki wa kizazi kipya kama Juma Nature, Profesa Jay na Dullayo, Nazir Khalifani na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’  limeongeza mkakati mwingine wa kutafuta chipukizi wa muziki wa kizazi kipya.

    Akizungumza na bongostaz, Mratibu wa bonanza hilo Mussa Chimae, amesema lengo lilikuwa kusaidia watoto wenye ulemavu wa akili kwa ajili ya kushiriki michezo ya Olimpiki kwa walemavu, lakini wameamua kuongeza jambo jingine.

    “Tulilenga kusaidia watoto wenye ulemavu wa akili, ambao wanatarajiwa kushiriki michezo ya Olimpiki kwa upande wa walemavu, lakini tumeona tuongeze na jambo jingine ambapo tutatafuta vijana wenye vipaji vya kuimba muziki,” alisema Chimae.

    Chimae alisema bonanza hilo litakalowahusisha wasanii na wachezaji mbalimbali kutoka mikoa ya Kusini litafanyika kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

    “Kwa kuwa ndio tunaanza kufanya bonanza hili kwa mara ya kwana tutafanya kwenye Mkoa wa Mtwara tu, lakini tukiona linamafanikio tutafanya na mikia mingine ya kusini,” aliongeza Chimae.

    Moja ya mambo yatakayofanyika kwenye bonanza hilo ni pamoja na burudani na mchezo wa soka kati ya maveterani wa Mkoa huo wa Mtwara na wasanii na wachezaji wa kutoka mikoa hiyo ya kusini.

    Pamoja na akina Juma Nature na Profesa Jay, wengine ni Z Anto, Jafaray, KR Mullah, Kaka Man, D Knob, huku upande wa wacheji ukiwa na akina Aliphonce Amlima, Mmachina, Nizar na Salvatory Ibrahim.

    Nizar Khalfan ametemwa na klabu ya Philadelphia Union ya Ligi Kuu ya Marekani mwezi uliopita na sasa hana timu.

    Alitemwa na klabu hiyo miezi mitatu tu tangu achukuliwe baada ya kufuzu majaribio.

    Nizar alikwenda kufanya majaribio Union, baada ya kutemwa na Vancouver, Novemba 23, mwaka jana.

    Nizar aliyezaliwa Juni 21, mwaka 1988 mjini Mtwara, alijiunga na Vancouver Whitecaps FC ya Canada Agosti 22, mwaka 2009 akitokea Moro United ya Ligi Kuu ya Bara na akacheza mechi tisa msimu wa kwanza wa 2009 na kuongezewa mkataba wa kuichezea timu hiyo msimu uliofuata wa 2010.

    Alifunga bao lake la kwanza Whitecaps Juni 12, mwaka 2010 katika mechi dhidi ya Austin Aztex na haikushangaza Februari 9, mwaka jana aliposaini mkataba mpya wa mwaka mmoja baada ya timu hiyo kupanda Ligi Kuu ya Marekani, maarufu kama Major League Soccer.

    Hata hivyo, baada ya msimu huo timu yake ikirejea Daraja la kwanza, Niazar akatemwa na kwenda Philadelphia Union, ambako miezi mitatu baadaye ametemwa nako.

    Juhudi za kumpata Nizar kuzungumzia mustakabali wake zinaendelea.

    Kabla ya Moro United, Nizar aliyeibukia kwenye timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2004, alichezea

    Mtibwa Sugar FC, na baadaye akanunuliwa na Al Tadamon ya Ligi Kuu ya Kuwait msimu wa 2007-2008.

    Januari 2008 aliondoka Al Tadamon na kusaini mkataba na Tadamon Sour ya Lebanon, ambako alipomaliza mkataba wake akarejea Tanzania kuchezea Moro United.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIZAR AIBUKIA SOUTH STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top