• HABARI MPYA

    Monday, May 07, 2012

    BOCCO ADEBAYOR ATWAA TUZO MBILI USIKU HUU


    John Bocco kushoto, akiwa Said Mourad kulia aliyeshinda tuzo ya mchezaji aliye fiti zaidi Azam msimu huu

    JOHN Raphael Bocco maarufu kama Adebayor leo amefunga bao moja katika ushindi wa 2-1 wa Azam katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na kutwaa kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kufikisha mabao 19.
    Bocco amempiku mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi aliyemaliza na mabao 12 na hivyo kufanya kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu kiweke maskani Chamazi kwa msimu wa pili mfululizo, kwani msimu uliopita alitwaa mchezaji wa Azam pia, Mrisho Ngassa.
    Azam pamoja na kumpongeza Bocco kwa mchango wake huo mkubwa uliowezesha klabu kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, pia wamemtangaza kwamba ndiye mchezaji bora wa msimu wa klabu hiyo.
    Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo, iliyofanyika hoteli ya JB Belmonte katikati ya Jiji, Mwenyekiti wa Azam FC, Abubakar Bakhresa alisema kwamba wanampongeza Bocco kwa mchango wake na wanamuomba aongeze juhudi.
    Awali kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Agetile Osiah Malabeja alisema kwamba wanavutiwa sana na Bocco kwa nidhamu yake na kujituma- lakini akamuomba abadilishe uamuzi wake wa kujiuzulu kuchezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa sababu yeye bado ni kijana mdogo na taifa linahitaji mchango wake bado.
    Bocco alifikia uamuzi wa kujiuzulu Stars kutokana na kuzomewa na mashabiki kwa sababu anakosa sana mabao.
    Lakini wadau wengi wamekuwa wakimsihi abadilishe uamuzi wake na kurejea kwenye timu- ili afanyie kazi mapungufu yake na siku moja atakuwa kinara wa mabao wa timu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO ADEBAYOR ATWAA TUZO MBILI USIKU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top