HUWEZI kuzungumzia makipa waliowahi
kung’ara zaidi duniani, bila kumtaja na Dino Zoff (pichani kushoto) wa Italia aliyezaliwa
Februari 28, mwaka 1942 mjini Mariano del Friuli.
Kipa huyo wa zamani wa kimataifa wa Italia,
amewahi kuidakia Azzuri hadi kuiwezesha kutwaa Kombe la Dunia, akiwa na Nahodha
wa kikosi hicho mwaka 1982 katika fainali zilizofanyika nchini Hispania, wakati
huo akiwa ana umri wa miaka 40 na miezi minnena siku 13.
Zoff alikuwa kipa wa uhakika, mwenye uwezo
mkubwa wa kuokoa michomo kiasi kwamba aliteuliwa kuwa kipa namba tatu kwa ubora
duniani kihistoria katika karne ya 20, nyuma ya Lev Yashin na Gordon Banks.
Anashikilia rekodi ya kusimama langoni muda
mrefu zaidi bila kuruhusu bao katika michuano ya kimataifa, akiwa amesimama
kwenye milingoti mitatu dakika 1142 kati ya mwaka 1972 na 1974 bila kwenda
kuokota mpira nyavuni.
Akiwa amedeaka mechi 112, anashika nafasi
ya tatu nyuma ya Fabio Cannavaro na Paolo Maldini katika kucheza mechi nyingi
zaidi kwenye kikosi cha Azzurri.
Mwaka 2004, Pele alimuingiza kipa huyo
katika orodha ya wanasoka ‘babu kubwa’ 125 kuwahi kutokea duniani.
Dino Zoff alizaliwa Mariano del Friuli,
Friuli-Venezia Giulia nchini Italia na kisoka alianza kuibuka akiwa ana umri wa
miaka 14 alipokuwa akifanya majaribio kwenye klabu ya Inter Milan na Juventus
F.C., kabla ya kupigwa chini kutokana ufupi wake.
Miaka mitano baadaye akiwa ameongezeka
urefu kwa sentimita 33, alifanikiwa
kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A akiwa na klabu ya
Udinese, ingawa katika kipindi chote cha kuwa na klabu hiyo Zoff alicheza mechi
nne tu kabla ya kutimkia Mantova mwaka 1963.
Mwaka 1968, Zoff alihamishiwa Napoli. Mwaka
huo huo, aliichezea Italia mechi ya kwanza katika mechi dhidi ya Bulgari, ikiwa
ni Robo Fainali ya ya Euro mwaka 1968.
Alianza vizuri kwa kuiwezesha Italia kutwaa
taji hilo nyumbani, Zoff baada ya kucheza mechi nne tangu hapo.
Aliachwa katika kikosi cha kwanza cha
Italia kilichocheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1970, ingawa Zoff alirejea
kwenye mafanikio baada ya kusaini Juventus mwaka 1972.
Katika miaka 11 ya kuwa na Juventus, Zoff
alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia, Serie A mara sita, Coppa Italia mara
mbilina Kombe la UEFA mara moja.
Hata hivyo, mambo makubwa zaidi Zoff
aliyafanya katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982, akiwa Nahodha wa Italia
alipoiwezesha kutwaa taji hilo katika umri wa miaka 40, akiweka rekodi ya kuwa
kipa mzee zaidi kutwaa ubingwa wa dunia wa kandanda.
Alifuatia mafanikio ya Giampiero Combi,
kuwa kipa wa pili kuwa Nahodha wa kikosi cha ubingwa wa Dunia.
Aidha, alichaguliwa pia kuwa kipa bora wa
michuano hiyo na kocha wa kikosi hicho, Enzo Bearzot alisema; “Alikuwa kipa wa
kiwango cha juu mno, alifanya shughuli nzuri sana akiokoa michomo ya hatari na
kuisaidia timu. Mwishoni mwa mchezo dhidi ya Brazil, alikuja kunipiga busu
shavuni, bila kusema neon lolote. Kwangu, ulikuwa wakati mzuri sana katika
Kombe la Dunia,”.
Zoff, Gianpiero Combi na Iker Casillas
aliyeiwezesha Hispania kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 hao ndio makipa pekee
hadi sasa kuwa Manahodha wa vikosi vya ubingwa wa Kombe la Dunia. Rekodi yake
ya kutofungwa muda mrefu katika mechi za kimataifa ilitibuliwa na mchezaji wa
Haiti, Manno Sanon aliyemtungua bao tamu katika fainali za Kombe la Dunia mwaka
1974.
Anashikilia pia rekodi ya kuwa mchezaji
‘mzee’ zaidi kucheza Serie A na pia alikuwa anashikilia rekodi ya kucheza mechi
nyingi zaidi kwenye ligi hiyo, akiwa amedaka mechi 570 kwa miaka zaidi ya 20,
hadi msimu wa 2005–2006 rekodi hiyo ilipovunjwa na kipa wa S.S. Lazio, Marco
Ballotta na beki wa A.C. Milan, Paolo Maldini.
Baada ya kustaafu soka, Zoff kama wanasoka
wengi wengine alihamia kwenye ukocha, akiingia kwenye benchi la ufundi la klabu
ya Juventus, ambako aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu kuanzia mwaka 1988 hadi 1990.
Mwaka 1990 alitupiwa virago, licha ya
kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la UEFA. Akajiunga na Lazio, ambako
aliteuliwa kuwa rais wa klabu hiyo mwaka 1994.
Mwaka 1998, Zoff aliteuliwa kuwa kocha wa
timu ya taifa ya Italia, akitambulisha mfumo wa kushambulia ‘mwanzo mwisho’,
ambao haswa ndio mfumo wa Azzuri na aliiwezesha timu hiyo kuwa mshindi wa pili
kwenye Euro mwaka 2000.
Alikaribia kutwaa taji kama si Ufaransa
kupata bao la kusawazisha dakika za majeruhi kwenye fainali. Siku chache
baadaye Zoff alijiuzulu, kutokana na kutupiwa ‘madongo’ na rais wa A.C. Milan,
Silvio Berlusconi aliyekuwa pia Waziri Mkuu wa Italia, ambaye naye hivi
karibuni amejiuzulu nafasi yake ya kisiasa kwa shinikizo la wananchi.
Zoff alirejea Lazio, lakini alistaafu
kutokana na matokeo mabaya mwanzosni mwa msimu wa 2001–2002. Mwaka 2005,
alipewa Ukocha wa Fiorentina.
Lakini baada ya kuwasaidia kuepuka kushuka
daraja siku ya mwisho ya msimu, Zoff alionyeshwa mlango wa kutokea. Kwa
muhtasari huyo ndiye Dino Zoff, kipa mwenye rekodi kibao za kipekee duniani.
WASIFU WAKE:
JINA: Dino Zoff
KUZALIWA: Februari 28, 1942 (Miaka 69)
ALIPOZALIWA: Mariano del Friuli, Italy
NAFASI: Kipa
KLABU ALIZOCHEZEA:
Mwaka Klabu
1961–1963 Udinese
(Mechi 38)
1963–1967 Mantova
(Mechi 131)
1967–1972 Napoli
(Mechi 143)
1972–1983 Juventus
(Mechi 330)
JUMLA: Mechi 642
(Tangu 1968 hadi 1983 aliidakia Italia
mechi 112)
TIMU ALIZOFUNDISHA:
1988–1990 Juventus
1990–1994 Lazio
1996–1997 Lazio
1998–2000 Italia
2001 Lazio
2005 Fiorentina
0 comments:
Post a Comment