![]() |
Marehemu Socrates |
WAPENZI wa soka duniani walizipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa gwiji wa zamani wa soka nchini Brazil, Socrates
aliyefariki dunia Desemba 4, mwaka jana akiwa ana umri wa miaka 57.
Utanashati wake na kitendo chake cha
kujiingiza kwenye siasa kwa undanikilimfanya awe mtu wa kipekee katika soka ya
Brazil, akijitofautisha mno na wasanoka wa enzi zake hata wa sasa.
Alifahamika zaidi pale alipokuwa Nahodha wa
kikosi cha Brazil katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982, ikichukuliwa na
wengi kama timu bora daima ya Brazil ambayo haikuwahi kutwaa taji kubwa la
michuano ya kandanda.
Lakini pia alikuwa maarufu mno kwa
kuutandika mtindi, yaani kilevi, jambo ambalo inaelezwa limechangia kifo chake
katika umri huo.
Taarifa kutoka hospitali ya Albert Einstein
ilisema kwamba Socrates alifariki kutokana na mshituko majira ya saa 4:30
asubuhi saa za Brazil.
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff alisema
Brazil imepoteza mmoja wa watoto wake adimu.”
“Ndani ya Uwanja, kwa kipaji chake na
harakati zake, alikuwa mweledi,” alisema katika taarifa yake. “Nje ya Uwanja, …
alikuwa mwanasiasa haswa, aliyejihusisha na nchi yake na watu wake.”
Rais wa zamani, Luiz Inacio Lula da Silva
pia alielezea machungu yake kutokana na msiba huo.
“Socrates’ alikuwa ana mchango mkubwa kwa
Corinthians, kwa soka na jamii ya Wabrazil haitaweza kumsahau daima,” alisema
Silva, mpenzi wa Corinthians, klabu ambayo Socrates aliichezea miaka ya 1980.
Socrates alikimbizwa hospitali siku chache
kabla ya kifo chake akiwa mwenye hali mbaya na kuwekewa uangalizi maalum. Hiyo
ilikuwa mara ya tatu ndani ya miezi minne kwake kulazwa hospitalini chini ya
uangalizi maalum, mara ya mwisho ikiwa Septemba, mwaka jana.
Mara mbili za mwanzo ilielezwa kwamba
alikuwa ana tatizo lililosababishwa na presha ambayo ilitokana na damu
kubadilisha mwelekeo wake na kuelekea kwenye ini.
Socrates hakuwahi kukanusha tuhuma za
‘ulevi mbwa’ enzi zake akicheza miaka ya 1980, lakini alisema aliacha
kuutandika mtindi mapema mwaka jana baada ya kufikishwa hospitali.
“Socrates alionekana kama mchezaji wa
zamani nyingine,” alisema mshambuliaji wa zamani wa Italia, Paolo Rossi. “Huwezi
kumuweka katika kipengele chochote — ndani na nje ya Uwanja.
Kila mmoja alijua juu ya Shahada yake
katika dawa za tiba za wanadamu na alikuwa ana tamaduni nyingi na
aliyejihusisha na mambo ya kijamii pia. Alikuwa wa kipekee kwa kila mtazamo.”
Socrates aliangukia kwenye udaktari baada
ya kustaafu soka na baadaye akwa mchambuzi na mwana safu maarufu wa kwenye TV,
wakati wote akiwa mwenye mawazo ya kipekee na maoni ya kutatanisha.
Tangu zake za kucheza, Socrates hakuwahi
kukaa nayo moyoni mawazo yake ya kisiasa, alikuwa akiandika kwenye safu yake.
Alifahamika kama Dk. Socrates kwa sababu ya utaalamu wake dawa, na alikuwa
hodari wa kufanya mahojiano na vyombo vya habari.
Akiwa Corinthians, Socrates alianzisha
harakati za kutetea haki za wachezaji katika klabu hiyo zilizojulikana kama
Corinthians Democracy.
Mweledi huyo alikuwepo kwenye kikosi cha
Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico, lakini
zilikuwa fainali za mwaka 1982 nchini Hispania aliweka historia akiwa na
Brazil, ambayo Brazil pamoja na kuwa na kikosi kikali zaidi kihistoria
haikushinda taji.
Akiwa na wachezaji kama Zico na Falcao,
walifungwa na Italia 3-2 katika Raundi ya Pili licha ya kuhitaji sare tu ili
watinge Nusu Fainali.
Kifo chake kiliwahuzunisha wengi wakiwemo
wachezaji wenzake kama Rossi, ambaye alifunga mabao matatu peke yake katika
mechi hiyo.
Wachezaji kibao wa Brazil wameelezea
majonzi ya kutokana na msiba huo.
“Machungu ni tangu siku ile,” alisema
mshambuliaji mstaafu wa Brazil, Ronaldona kuongeza. “Pumzika kwa amani Dk.
Socrates.”
Socrates aliandika makala kibao katika safu
yake wakati wa michuano ya Copa America nchini Argentina mwaka jana, akielezea
maoni yake kuhusu mashindano hayo, ikiwemo suala la kiuchumi na masuala ya
kisiasa Latin America.
Socrates, ambaye jina lake halisi ni
Socrates Brasileiro Sampaio de Souza Vieira de Oliveira, pia alichezea klabu za
Flamengo and Santos.
Socrates alikuwamo kwenye orodha ya
wanasoka 125 bora wanaoishi ya FIFA, orodha ambayo ilitayarishwa na gwiji
mwingine wa zamani wa Brazil, Pele.
Socrates aliichezea mechi 63 timu ya taifa
ya Brazil na kuifungia mabao 25.
Socrates pia aliifundisha na kuichezea kwa
muda mfupi klabu ya Garforth Town nchini England mwaka 2004.
Mdogo wa Socrates, Rai alikuwa kiungo
mahiri wa Brazil na aliisaidia timu hiyo kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1994
Marekani.
Mazishi yake yalifanyika nyumbani kwao
Ribeirao Preto, huko Sao Paulo na ameacha mke na watoto sita. Mungu aiweke pema
peponi roho ya marehemu. Amiiin.
WASIFU WAKE:
JINA KAMILI: Sócrates Brasileiro Sampaio de
Souza Vieira de Oliveira
KUZALIWA: Februari 19, 1954
ALIPOZALIWA: Belém do Pará, Brazil
KUFARIKI DUNIA: Desemba 4, 2011 (Miaka 57)
ALIPOFIA: São Paulo, Brazil
NAFASI YAKE: Kiungo mshambuliaji
TIMU ALIZOCHEZEA:
Mwaka Timu
1974–1978 Botafogo-SP
(Mechi 57, mabao 24)
1978–1984 Corinthians (Mechi 297, mabao172)
1984–1985 Fiorentina (Mechi 25, mabao 6)
1986–1987 Flamengo (Mechi 11, mabao 3)
1988–1989 Santos (Mechi 5, mabao 2)
1989 Botafogo-SP
(Aliishia kusugua benchi)
2004 Garforth
Town (Mechi 1, bao 1)
JUMLA) (Mechi
396, mabao 207)
(Tangu 1979 hadi 1986, aliichezea Brazil
mechi 60, akaifungia mabao 22)
0 comments:
Post a Comment