OOH SAJUKI! Siku mbili kabla ya kwenda
katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu, afya ya stadi wa filamu
za Kibongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ni ya kusikitisha kupitiliza.
Kadiri siku zinavyosonga, hali ya Sajuki
inazidi kuwatoa watu machozi baada ya kuzidiwa na kushindwa kunyanyuka
kitandani. Laiti kama utamuona na ukashindwa kububujikwa na machozi basi
utakuwa huna utu.
ASHINDWA KUPOKEA MCHANGO
Tukio bichi kabisa lililowatoa machozi
wasanii wenzake ni lile la Jumanne wiki hii nyumbani kwake Tabata Barakuda, Dar
es Salaam ambapo msanii na prodyuza huyo wa filamu alishindwa kuamka kitandani
kupokea dola elfu kumi (takribani Sh. milioni 15) alizozitoa mwigizaji
mwenzake, Jacqueline Wolper kwa ajili ya matibabu huku akisindikizwa na mastaa
wengine wa Bongo Movie.
The Udaku Master, Ijumaa lilimshuhudia
Sajuki akiugulia maumivu huku akilalamika kujisikia vibaya, hivyo kuwaomba
wasanii wenzake kwa heshima waingie chumbani kwake ili apokee fedha hizo.
WASANII VILIO
Kitendo hicho ndicho kilichowafanya baadhi
ya wasanii wenzake kushindwa kujizuia na kujikuta wakiangua vilio huku Sajuki
akiwatuliza na kuwaomba wasilie wala wasihuzunike kwani kila kitu ni mapenzi ya
Mungu.
“Msihuzunike ndugu zangu, naamini kila kitu
ni mapenzi ya Mungu na si vinginevyo, jipeni moyo,” alisema Sajuki kwa tabu
akiwa amelala kitandani akiwa amezungukwa na mastaa hao.
WOLPER
Kwa upande wake Wolper aliyekuwa akimwaga
machozi mithili ya bomba la mvua, alisema kuwa siyo kwamba ana fedha nyingi,
ila ni namna alivyoguswa na mateso ya Sajuki.
“Siyo kwamba sina shida bali ni moyo wa
kusaidia kuokoa uhai wa mwenzetu. Tulizoea kuwa naye location (sehemu ya
kurekodia filamu) na kwenye tasnia yetu, anaumwa na hajiwezi, niliumia sana,”
alisema Wolper aliyekuwa akifutwa machozi na wenzake.
WASTARA
Naye mke wa Sajuki, Wastara Juma, huku
akilia muda wote, alitoa shukurani zake za dhati kwa Wolper na kueleza jinsi
alivyoguswa na kuona umuhimu wa kumsaidia mumewe.
MASTAA
Baadhi ya mastaa wa Bongo Movie
walioambatana na Wolper kuwasilisha mchango huo ni pamoja na Jacob Steven ‘JB’,
Muhsein Awadhi ‘Dk. Cheni’, Chiki Mchoma ‘Chiki’, Hartmann Mbilinyi, Sabrina
Rupia ‘Cathy’ na wengine.
TUMEFIKAJE HAPA?
Oktoba, 2011, magazeti ya Global Publishers
yalikuwa ya kwanza kuripoti habari ya Sajuki kuwa hoi kitandani akipatiwa
matibabu katika Hospitali ya TMJ, Dar.
Katika mahojiano yake, Sajuki aliyaambia
magazeti ya Global: “Madaktari walibaini nina uvimbe pembeni ya ini. Ni tatizo
ambalo limekuwa likinisumbua kwa muda mrefu.
“Kwa siku za hivi karibuni nimekuwa siwezi
kuamka kitandani kwani napata maumivu makali kupita maelezo, hivyo nasubiri
kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya TMJ.”
HISTORIA UGONJWA WA SAJUKI
Taarifa za awali kabla ya Sajuki
kuthibitisha ilielezwa kuwa alianza kwa kupata uvimbe sehemu tofauti katika
mkono wake mmoja lakini baadaye tatizo hilo lilihamia ndani na kuanza kupata
maumivu makali pembeni ya ini.
UNDANI WA UGONJWA
Kwa mujibu wa daktari aliyezungumza na
Ijumaa (jina linahifadhiwa kwa sababu maalum), uvimbe pembeni ya ini ni dalili
za ugonjwa alioutaja kitaalamu kama Hepatoma.
HEPATOMA NI NINI?
Daktari huyo alieleza kuwa Hepatoma ni moja
ya kansa za ini ambayo huanzia kwenye sehemu ya juu kulia ya ini.
CHANZO
Ilifahamika kuwa chanzo cha Hepatoma ni
magonjwa yanayoshambulia ini kwa pamoja, kitaalamu huitwa Hepatitis. Mbali na
magonjwa hayo shambulizi, pia watu wanaotumia pombe, madawa ya kulevya wapo
hatarini zaidi kupatwa na ugonjwa huo.
DALILI
Dalili za Hepatoma ni pamoja na maumivu
makali sehemu ya juu ya kulia ya ini, kupoteza hamu ya kula, kukosa usingizi,
kukondeana na kukosa furaha, yaani mtu wa ‘stresi’ muda mwingi.
MATIBABU
Mara nyingi njia ya upasuaji huwa chaguo la
kwanza ili kuundoa uvimbe, dozi maalumu ya kutibu uvimbe huo na dawa za
kutuliza maumivu.
KILA LA HERI SAJUKI
Timu ya Ijumaa na Wafanyakazi wa Kampuni ya
Global Publishers, wanawatakia Sajuki na Wastara safari njema ya matibabu
nchini India watakapoondoka Jumapili ijayo.
Tunaamini watarejea na matumaini tele kwani
tunawasubiri kuwaona runingani wakituburudisha tunapokuwa sebuleni kwetu.
Mbali
na dua za Watanzania kwa namna kila mtu anavyoguswa, tunaomba tuendelee
kumchangia fedha kupitia simu ya mkononi kwa kutuma kwenye Tigo Pesa namba 0713
666 113 au kwenye akaunti namba 050000003047 katika Benki ya Akiba Commercial
yenye jina la Wastara Juma Issa-Mhariri..
0 comments:
Post a Comment