![]() |
Emanuel Okwi wa Simba, mmoja wa wachezaji waliong'ara Ligi Kuu Bara |
BAADA ya miezi nane ya patashika ya Ligi
Kuu ya Tanzania Bara, kesho ligi hiyo inafikia tamati kwa timu zote 14 kushuka
dimbani kwenye viwanja tofauti, huku kivutio kikubwa kikiwa mchezo wa watani wa
jadi Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu na
mashabiki wa soka, na sababu kubwa ni kwamba, matokeo ya mechi hiyo yanaweza
kuwa seheme ya kutoa bingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Mechi nyingine za kesho ni Oljoro JKT
itakayoikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid,
Arusha wakati Ruvu Shooting itacheza na Villa Squad kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Aidha, Coastal Union itacheza na Toto
African Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku African Lyon ikicheza na JKT
Ruvu kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.
Timu ya Azam itaikaribisha Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam na Moro United itakuwa ikicheza
na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kimahesabu, ni timu za Simba na Azam ndizo
zenye nafasi ya kutwaa ubingwa ulioachwa wazi na Yanga.
Kwa mujibu wa kanuni namba 4(2)(c) ya Ligi
Kuu, timu tatu za mwisho katika msimamo wa ligi zitashuka daraja, ambapo tayari
Moro United na Polisi Dodoma zimeshashuka, iliyobaki itajulikana baada ya mechi
za kesho ambazo zote zitaanza saa 10 kamili jioni ili kuepuka upangaji wa
matokeo.
Katika hali halisi ya uendeshaji ligi,
hakuna msimu uliowahi kupita bila kuwapo na upungufu, na ndivyo ilivyokuwa
msimu huu unaofikia tamati kesho, ambapo tumeshuhudia malalamiko chungu mzima.
Pamoja na kuwapo na malalamiko kila msimu,
lakini kile kilichoshuhudiwa msimu huu, kimeonyesha sura mpya jinsi ligi hii
inavyoendeshwa bila mpangilio wenye heshima ya mchezo wa soka.
Tatizo kubwa linaloendelea kuzungumzwa
mpaka sasa, ni suala la waamuzi ambao wamekuwa wakilalamikiwa kila kona kwa
sababu ya, aidha kuchezesha kwa upendeleo au kutosimamia ipasavyo sheria za
mchezo huo.
Ingawa hatuwezi kukubali moja kwa moja
malalamiko yote yaliyoelekezwa kwao waamuzi yalikuwa na msingi, lakini bado pia
hatuwezi kuficha ukweli kwamba hakukuwa na upungufu.
Eneo lingine lililoongoza kupokea
malalamiko ni kamati mbalimbali za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambazo
kuna wakati zilipinga waziwazi katika kutoa uamuzi wa masuala kadhaa
yaliyoletwa mezani kujadiliwa.
Kutokana na udhaifu wa kiutendaji wa kamati
hizi, ilifika wakati zililazimika kuuleta mchezo wa soka mezani na kutoa
matokeo badala ya viwanjani kama taratibu zinavyoonyesha.
Kwa jumla kamati hizi zilivuruga sana ligi,
ziliwachanganya wadau na wapenzi wa soka na pia zilichangia kushusha heshima ya
mchezo wa soka kwa kufuta matokeo ya uwanjani na kutoa matokeo ya mezani.
Hakuna shaka kwamba, kwa aina ya uamuzi
uliokuwa ukitolewa na kamati hizi katika mambo mbalimbali waliyojadili, wadau
wamepoteza imani na utendaji wake.
Lakini pia suala la usalama kwenye viwanja
nalo ni tatizo kubwa msimu huu, ambapo mara nyingi tumeshuhudia mashabiki
wakifanya uharibifu kwenye Uwnaja wa Taifa hasa kwenye mechi zinazohusu timu za
Simba na Yanga.
Aibu nyingine kubwa ni kukosekana kwa
magari ya huduma ya kwanza viwanjani kwa ajili ya kutoa usafiri wa haraka
kwenda hospitali iwapo kutakuwa na tatizo lolote.
Isitoshe, viwanja vilivyotumika katika
mechi za ligi navyo vimelalamikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa chini ya
kiwango kwa mashindano makubwa kama ya Ligi Kuu.
Tumeona pia upungufu wa utawala bora kwa
baadhi ya viongozi wa timu za Ligi Kuu uliopelekea baadhi ya makocha kuacha
kufundisha timu hizo.
Baadhi ya viongozi wa klabu wamekuwa chanzo
kuendesha klabu bila kuzingatia kanuni, jambo ambalo mara kwa mara limekuwa
likileta maelewano finyu kati ya wanachana na viongozi.
Tunaamini TFF na klabu zetu za soka zimeona
upungufu huu na hii iwe changamoto ya kufanya marekebisho ili msimu ujao ligi
iwe na sehemu kubwa ya ushindani kuliko kiyume chake.
TFF kwa kushirikiana na kamati zake,
inapaswa kukaa chini na kuweka mambo sawa, kwani sehemu kubwa ya malalamiko
toka kwa wadau msimu huu yanagusa moja kwa moja utendaji wa shirikisho hilo.
GAZETI LA MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment