Beki Chacha Marwa wa Yanga kulia, katika moja ya mechi Ligi Kuu |
MASHINDANO yoyote yale ili yaendeshwe kwa
ufanisi na ushindani wa haki ni lazima yawe na kanuni. Na si tu kuwa na kanuni,
bali pia ziwe zinaeleweka kwa wahusika.
Kama ilivyo kwa Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nalo linaendesha
mashindano yake kwa kutumia kanuni. Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara ina kanuni zake kama ilivyo kwa Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya
Taifa, Kombe la Taifa, michuano ya Copa Coca Cola na mingineyo.
Ili timu iwe mshiriki na mshindani wa kweli
katika michuano hiyo ni lazima iwe na ufahamu katika michuano husika. Ni rahisi
timu kupoteza ushindi, kupigwa faini na hata kupokwa haki ikiwa haina ufahamu
wa kanuni.
Kama timu inashiriki mashindano halafu haifahamu
kanuni za mashindano husika inawezaje kuwa mshindani wa kweli? Ni kawaida kwa
klabu za Tanzania katika ngazi mbalimbali, hata mashindano ya kugombea mbuzi kuingiza timu
bila kuomba, kupewa au kutaka kufahamu kanuni kwa mashindano husika.
Hali hiyo husababisha vurugu katika
mashindano kwa vile timu inaposhindwa mechi hulalamikia vitu vingine ambavyo
kwa mujibu wa kanuni havikupaswa kulalamikiwa, lakini kwa upofu wa kanuni timu
au klabu hulalamika.
Hufika mahali klabu inaelekeza nguvu katika
malalamiko au rufani kuliko kuwekeza katika timu ili iweze kufanya vizuri,
ambapo matokeo yake ni kutokuwepo ushindani kutoka kwa timu husika au
mashindano yenyewe kwa ujumla.
Katika TFF chombo chenye mamlaka ya
kupitisha au kurekebisha kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom ni Kamati ya Utendaji.
Hata hivyo ni utaratibu wa TFF kukaa na klabu za Ligi Kuu kila yanapofanyika
marekebisho kabla ya kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Utendaji.
Mfano Kanuni ya 61 kuhusu kocha wa timu
inasema: “(1) Klabu inapaswa kuajiri kocha wa timu mwenye ujuzi wa kutosha na
anayetambuliwa na Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA), na mkataba wake
kusajiliwa TFF.
“(2) Kocha klabu ya Ligi Kuu anatakiwa awe
na Stashahada au cheti cha ngazi pevu ya ufundishaji. (3) Kocha kutoka nje
atathibitishwa na TFF kabla ya kuingia mkataba na klabu na kupewa kibali cha
kuishi na kufanya kazi nchini.
“(4) Kocha atatakiwa kuwa na leseni daraja
A kutoka TFF kuweza kufundisha klabu ya Ligi Kuu. (5) Kocha wa timu ndiye mkuu
wa shughuli zote za timu kuanzia usajili wa wachezaji, uandaaji wa timu, usimamiaji katika
mashindano na mambo mengine yanayofanana na hayo.”
Ni kocha wa sifa za aina gani anaweza
kufundisha timu ya Ligi Kuu na kwa utaratibu upi. Kanuni hiyo ya 61 imeelezea
hayo kwa lugha nyepesi na inayoeleweka. Lakini pamoja na kanuni kuwa wazi, bado
ni kawaida katika klabu za Ligi Kuu kusikia matatizo kadha wa kadha kuwahusu makocha ambao ni muhimu katika
timu zao katika utengenezaji wa aina ya uchezaji.
Kwa kifupi aina ya uchezaji au mfumo wa
uchezaji hupangwa au uamuriwa na kocha kutokana na aina ya wachezaji alionao, lengo siku
zote ikiwa ni kuhakikisha timu inacheza vizuri. Mara nyingi matokeo ya kucheza
vizuri ni ushindi.
Licha ya kanuni kama hizo kutengenezwa bado
yamekuwepo matatizo kwa makocha. Je, ni kipi chanzo cha matatizo hayo? Ukweli
unabaki kuwa kutojua au kutozingatia kanuni ndiyo msingi wa migogoro
isiyokwisha inayohusu makocha kwa upande mmoja na viongozi wa klabu kwa upande
mwingine.
Kanuni hiyo inayohusu makocha ni mfano tu
kuonesha jinsi wadau wa mashindano husika walivyokosa umakini katika suala la
msingi kama hilo. Kanuni ndiyo mwongozo wa kila kitu katika mashindano.
Timu ikitaka iharibikiwe katika mashindano
iache kuzingatia kanuni. Pia ikumbukwe kuwa kanuni zote katika mashindano ni
sawa. Dhana kuwa kanuni hii ndiyo mama na ya msingi si sahihi hata kidogo, kwa
vile kanuni zote zimewekwa au kutengenezwa kwa sababu maalumu.
Ndiyo maana huwezi kukuta kanuni inayohusu
Kombe la Dunia kwenye Ligi ya Taifa. Hiyo ni kutaka kuonesha kuwa kila kanuni
ni muhimu kwa mashindano husika, hivyo haikutengenezwa kama mapambo.
Klabu inayowajibika ni ile inayozingatia
kanuni badala ya kufanya mambo kwa kubahatishakwa dhana kuwa wasimamizi wa mashindano au
klabu pinzani haiwezi kubaini ukiukwaji wa kanuni husika.
Ni kwa kucheza ligi huku tukifahamu kanuni
ndiko kutatufanya tuongeze msisimko na kuifanya ligi yetu kuwa bora, hivyo
kuvuta wadau wengine muhimu wa kurahisisha mambo yetu.
*Makala haya imeandikwa na Boniface Wambura
ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
0 comments:
Post a Comment