![]() |
Wachezaji wa Azam |
TUHUMA dhidi ya waamuzi kuchezesha kwa
upendeleo kunako ashiria mazingira ya rushwa sio za leo ni za muda mrefu sana.
Tuhuma za waamuzi kuchezesha chini ya
kiwango na kwa upendeleo wa wazi zimechukua sura mpya kwenye msimu huu wa Ligi
Kuu wa Soka Tanzania Bara kiasi cha kuonekana dalili njema ya suala lenyewe
kushughulikiwa au kupatiwa ufumbuzi kudumu.
Shukrani ziende kwa mmiliki wa klabu ya
Azam Said Salim Bakhressa kuanzisha timu hiyo inayoonekana kuzizidi nguvu za kifedha
miamba ya soka ya kihistoria nchini Simba na Yanga na ndio kiini cha kelele dhidi ya uamuzi
mbovu unaofanywa na waamuzi wa soka hapa nchini.
Kusingekuwepo timu yenye uwezo wa kifedha
kama ya Azam kwenye Ligi Kuu ni wazi malalamiko haya dhidi ya waamuzi
yasingefikia kiwango hiki kwani timu za Simba na Yanga zenye nguvu za kifedha zingeendelea
kupendelewa na mashabiki wa soka nchini wangeendelea kuziweka tuhuma hizi
kapuni.
Haihitaji elimu ya chuo kikuu kubaini kuwa
kama timu haina nguvu kubwa ya kifedha kama zilivyo Simba na Yanga suala la
kuwa bingwa wa soka wa Tanazania Bara ni kama ndoto, kwani hata rekodi za ndani
ya miaka 20 iliyopita zinaonesha timu hizo kubwa ndizo zilipokezana kutwaa
ubingwa huo.
Ukirudi nyuma kwenye miaka ya 1970 mpaka
mwanzoni mwa miaka ya 1980 kiwango cha uchezeshaji cha waamuzi kilikuwa bora
kidogo kutokana na maadili yaliyokuwepo kipindi hicho kiasi hata hao viongozi
wa Simba na Yanga ilikuwa nadra kutuhumiwa kuzihonga timu ndogo zichukue
ubingwa au hata waamuzi wenye kuzibeba timu kubwa.
Lakini kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980
mpaka sasa ndani ya nchi mpira umekuwa ukichezwa zaidi nje ya uwanja hasa na
timu hizi kubwa za Simba na Yanga kiasi cha kuzusha malalamiko ya mara kwa mara
toka kwa timu ndogo kuwa zinaonewa zinapocheza na timu hizo.
Lakini kwa kuwa timu hizo hazina uwezo
mkubwa wa kifedha malalamiko yao ya kuonewa na timu hizo kubwa hayakuwa
yanapewa uzito na matokeo yake soka la Tanzania linashuka kadiri miaka
inavyokwenda mbele.
Kupanda daraja na uwezo mkubwa wa kifedha
wa Azam sasa unaonekana kuwakera mashabiki na wadau wa soka nchini na kuzusha
tuhuma za rushwa dhidi ya timu hiyo, lakini ukweli ni kwamba nguvu za kifedha
za timu hiyo kwa sasa zinazidi za Simba na Yanga ndio kiini cha tatizo.
Azam imesajili wachezaji wenye uwezo mkubwa
na inaonekana imedhamiria hasa kulifanyia soka la Tanzania mabadiliko kutoka
kutawaliwa na Yanga na Simba kusikoleta tija kwa nchi hii.
Na tayari dhamira ya timu hiyo
imedhihirisha wazi kwani Yanga ambayo huwa ni mshiriki wa kudumu kwenye michuano ya kimataifa
mwakani haitashiriki michuano hiyo na sababu kubwa ni Azam.
Azam sasa inatoa presha kubwa kwa vinara wa
ligi hiyo Simba kwenye mbio za ubingwa na ikitokea ikashinda kwa idadi kubwa ya
mabao kwenye mchezo wake dhidi ya Mtibwa ulioamuliwa kurudiwa na ikaifunga
mabao mengi kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi Kagera Sugar na Yanga ikaifunga
Simba leo basi timu hiyo itakuwa bingwa.
Kama itakuwa bingwa Azam itakuwa imefanya
mambo mawili makubwa ambayo wadau wa soka wa nchi hii hawako tayari kuona
yanatokea kwanza kuinyima Yanga kushiriki michuano ya kimataifa na pili
kuinyima kigogo kingine cha soka nchi hii ubingwa yaani Simba.
Kwa hali hii ndio maana tuhuma dhidi ya
timu hiyo kuhonga waamuzi ndipo zinapoanzia kwa sababu imezibana timu vipenzi
za Watanzania walio wengi lakini wakati wadau wa soka hao wakirusha tuhuma hizo
kwa Azam wajichunguze na wao wenyewe na timu zao hizo wanazozipenda.
Kama wadau wa timu hizo ndio wameasisi
msemo wa mpira fitina wakiwa na maana ya ushindi huanza kupatikana kwa mipango ya
nje ya uwanja zaidi usafi wao uko wapi kiasi cha kuizonga na kuishambulia Azam.
Haya yanayosemwa kufanywa na Azam yamekuwa
yakisemwa kufanywa na Simba na Yanga muda mrefu sana, lakini hayakuwa kupata
mguso kutoka kwa wadau wa soka nchini zaidi ya kusikia wanasifia viongozi wao
kwa kujua fitina za mpira.
Iachwe Azam irekebishe soka la bongo kidogo
na ikibidi zitokee timu nyingine zenye uwezo kama wa Azam na ndipo umuhimu wa
wadau wa soka kujikana nafsi zao kwa kutafuta matokeo ya nje ya uwanja
utaonekana.
Imeandikwa na Clecence Kunambi wa gazeti la
Habari Leo..
0 comments:
Post a Comment