![]() |
Amir Mhando, Mwandishi wa Makala hii, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA |
YANGA inapita kipindi kigumu hivi sasa,
kipindi ambacho ni maumivu makubwa kwa mashabiki wake.
Hatua hiyo inatokana na timu hiyo kukosa
nafasi ya kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa mwakani inayoandaliwa
na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Tayari wana-Yanga wamegawanyika katika
makundi mawili, moja likiwashutumu viongozi na lingine likiwatetea kutokana na
kuvurunda kwa timu yao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inamalizika kesho, hali hiyo
inafanya ionekane kama kuna mgogoro, ambao kama wasipokuwa makini athari zake
zitakuwa kubwa.
Ilianza kama utani kwa wazee na baadhi ya
wanachama kuhoji mwenendo mbaya wa klabu yao, lakini hali ikafika pabaya wiki
iliyopita pale Baraza la Wazee la klabu hiyo lilipotangaza kwamba limechukua
timu na siku moja baadaye uongozi wa Yanga ukakanusha jambo hilo na kwamba timu
itaendelea kuwa chini ya uongozi.
Pande hizo mbili karibu wiki moja sasa
zimekuwa zikitupiana maneno ambayo yanaashiria hakuna amani, lakini
kilinichonisukuma zaidi kuandika makala haya ni kauli ya Jumanne wiki hii,
ambapo Baraza la Wazee lilitoa tamko kwamba kwa sasa limejiweka kando na kwamba
mambo ya Yanga yatabaki kuwa chini ya uongozi.
Wazee hawa hawakutoa kauli hiyo kwa nia
njema, bali wamesusa. Maana walifikia hatua mpaka ya kuvua kofia zao kuwalaani
viongozi wa Yanga, kwamba lolote litakalotokea wao halitawahusu.
Kwa lugha rahisi wazee hawa wamesema:
“Tutaona sasa kama watafanikiwa.” Ni kauli ambayo ukiwa na kiburi unaichukulia
kwa lugha rahisi na nyepesi, lakini ukiwa na busara unaiona ni nzito na yenye
kuhitaji busara zaidi ili kurudi katika msimamo mmoja.
Kwa mtazamo wangu wana- Yanga huu si wakati
wa kutengeneza migogoro, badala yake wajitahidi kwa kadri ya uwezo wao
kujiepusha nao kwani kauli hiyo ina maana kama Yanga itafanya vibaya basi wazee
wataibuka kidedea hasa kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Simba na kama Yanga
watashinda basi uongozi utakuwa umeibuka kidedea na hivyo heshima za wazee
zitakuwa zimetetereka.
Uzoefu wangu kunapokuwa na mgogoro katika
klabu za Simba na Yanga ni rahisi sana kuwahusisha hata wachezaji wa timu hiyo
na haikuwa ajabu miaka ya nyuma kusikia kuwa wachezaji wametekwa na upande
fulani katika mgogoro.
Mara nyingi sehemu panapokuwa hakuna umoja,
basi hata kufanya vizuri inakuwa nadra, hivyo lazima hili lifikiriwe kwa makini.
Kwa mtazamo wangu wazee wa Yanga
hawakupaswa kuchukua hatua ya kuwasusa viongozi, kwani binafsi naamini kumpiga
chura teke si kumkomoa, bali unamuongezea mwendo. Kama walifanya hivyo kwa
imani kwamba uongozi wa Yanga utatetereka hilo halipo, bali wenzao ndiyo
wamezidi kufurahia.
Ingekuwa vyema wazee wa Yanga
wangehakikisha wanakaa chini na uongozi kwa nia njema ya kujenga umoja kwa
maslahi ya Yanga.
Ufike wakati sasa klabu zifanye mambo
kisayansi zaidi badala ya kukurupuka katika jazba na chuki ambazo hazina msaada
wowote kwa maendeleo ya mchezo huo.
Hivyo kila hatua ambayo itachukuliwa na
kundi lolote ndani ya Yanga lazima itazamwe kwa umakini na upeo wa hali ya juu kwani
ninavyojua mimi Simba na Yanga, kila zinapofanya vibaya huwa hazikosi sababu
ambazo si za kitaalamu na zaidi ni kutupiana lawama zisizo na msingi.
Huwa naamini gari ya fundi makanika hailali
njiani ikipata matatizo, atajitahidi kuikorokochoa iendelee na safari.
Hivyo hata kwa Yanga wajitahidi kadri
wawezavyo kumaliza tatizo hili kwa pamoja. Kwa vyovyote iwavyo Yanga hawatakiwi
kususiana, kufanya hivyo si kuijenga timu lakini pia watambue kukimbia tatizo si suluhisho, bali
walikabili kwani mlevi huwa hasusiwi pombe, Nawasilisha.
0 comments:
Post a Comment