• HABARI MPYA

    Thursday, May 10, 2012

    MALAWI WAIPIGA TAIFA QUEENS




    TIMU ya taifa ya netiboli ya Tanzania ‘Taifa Queens’ jana ilishindwa kujisafishia njia baada ya kukubali kipigo cha mabao 33-30 dhidi ya mabingwa watetezi Malawi katika michuano ya mchezo huo ya Afrika.
    Katika mchezo huo mkali na wa kuvutia, uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, timu zote mbili zilitumia nguvu na ufundi wa hali ya juu.
    Malawi walianza kwa kasi mchezo huo na kuwaongoza wenyeji kwa magoli 13-6 katika robo ya kwanza.
    Baada ya kuona hivyo, kocha wa Tanzania, Mary Protas alilazimika kufanya mabadiliko robo ya pili kwa kumtoa mfungaji mrefu zaidi na Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 Mwanaidi Hassan na kumuingiza Pili Peter nafasi ya ufungaji (GS).
    Mabadiliko hayo yalikuwa ya kiufundi kutokana na Mwanaidi kutoelewana vema mfungaji msaidizi (GA), Irene Elias na yalizaa matunda hivyo timu kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 19-12.
    Baada ya mapumziko Tanzania ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Irene na kumuingiza Mwadawa Twalib kusaidiana na Pili katika ufungaji.
    Kadri mchezo ulivyosonga Taifa Queens ilionekana kuzinduka zaidi na kuwabana wapinzani wao hivyo hadi robo ya tatu kuendelea kubaki nyuma kwa tofauti ya magoli saba ambayo
    waliruhusu robo ya kwanza na kuwa nyuma kwa 27-20.
    Mabadiliko ya robo ya mwisho ya kumtoa Pili katika GS na kurudi Mwanaidi na Paskazia Kibayasa kuingia WD badala ya Restuta Boniface yalizaa matunda na hivyo kumaliza mchezo kwa mabao 34-30.
    Hata hivyo, kocha wa Tanzania, Protas alimlalamikia mwamuzi kutoka Lesotho, Chakatsa Lephole kuwa chanzo cha kipigo kwa timu yake hivyo kuwaacha njia panda katika mbio za kutwaa taji hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALAWI WAIPIGA TAIFA QUEENS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top