• HABARI MPYA

    Thursday, May 10, 2012

    SIMBA WAFIKA SALAMA SUDAN TAYARI KWA KAZI



    Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ''Kaburu' akiwa na Okwi Uwanja wa ndege jana Kaburu ataondoka kesho.
    Nahodha wa Simba, Juma Kaseja akihojiwa na Waandishi wa Habari Uwanja wa ndege jana.
    Kaburu akizungumza na Kaseja
    Wachezaji wa Simba wakiingia ndani Uwanja wa ndege tayari kwa safari

    TIMU ya soka ya Simba imefika salama usiku wa jana mjini Khartoum Sudan, tayari kwa mchezo wa mwisho mwa wiki wa marudiano, hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Simba liyoondoka Dar es Salaam jana alasir, inahitaji sare tu kwenye mchezo huo kusonga mbele, baada ya kushinda 3-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
    Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic alisema jana wakati timu hiyo ikiondoka kwamba kama vijana wake wakicheza vizuri hana hofu kwamba watawang’oa Wasudani na kusisitiza kuwa maandalizi yao wapo vizuri.
    Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano inayoandaliwa na CAF kwa ngazi ya klabu, ambapo wawakilishi wengine wa Tanzania ambao tayari wameshatolewa ni Yanga iliyotolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mafunzo iliyokuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje na Maqulmano ya Msumbiji.
    Nayo Jamhuri ya Pemba ilitolewa michuano ya Kombe la Shirikisho na Hwangwe FC ya Zimbabwe.
    Katika hatua hiyo inayofuata kama Simba itafuzu, itacheza na moja kati ya timu nane zitakazotolewa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikivuka hapo itaingia hatua ya makundi itakayohusisha timu nane zitakazokuwa kwenye makundi mawili tofauti.
    Simba imekwenda huko na wachezaji 19 na viongozi saba ambao ni Juma Kaseja, Ally Mustafa,
    Shomari Kapombe, Derick Walulya, Amir Maftah, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Kelvin Yondani, Victor Costa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango na Uhuru Selemani.
    Wengine ni Haruna Moshi, Machaku Salum, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Edward Shija na Gervais Arnold Kago, wakati viongozi ni Mwenyekiti Alhaj Ismail Aden Rage, Swedy Nkwabi, Cirkovic, Kocha Msaidizi Amatre Richard, kocha wa makipa James Kisaka, daktari Cosmas Kapinga, Meneja Nicholaus Nyagawa na Kamwaga.
    Mkuu wa msafara ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hussein Mwamba. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAFIKA SALAMA SUDAN TAYARI KWA KAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top