• HABARI MPYA

    Thursday, May 10, 2012

    NCHUNGA AUNGURUMA, TISA HATARINI KUTEMWA YANGA, MROMANIA KUMRITHI PAPIC


    Nchunga kulia

    MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga amesema hatajizulu na hawajibiki kwa wazee wachache wanaompiga fitina, bali wanachama.
    Gazeti la Mwananchi leo limeandika kwamba uongozi wa Yanga ukipuuza shinikizo zito la kutakiwa kujiuzulu toka baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kwa madai ya kuwa kiini cha kipigo cha aibu toka Simba Jumapili iliyopita, wachezaji tisa timu hiyo wamekalia kuti kavu baada ya mikataba yao kufikia.
    Wachezaji hao wako hatarini kutemwa kwa sababu kuna uwezekano mdogo, au usiwapo kabisa kusaini mikataba mipya, taarifa za ndani toka klabu hiyo ya Jangwani zimedai
    Ni pamoja na Shamte Ally, Jerry Tegete, Chacha Marwa, Mohamed Mbegu, Abuu Ubwa, Zuberi Ubwa,  Kigi Makasi, Shadrack Nsajigwa na Athuman Idd 'Chuji'.
    Tegete anahusishwa kwenda Simba, wakati Nsajigwa anatuhumiwa kucheza chini ya kiwango katika mechi yao dhidi ya Simba, ambapo alisababisha penalti mbili kati ya tatu na kuwapa mahasimu wao ushindi wa mabao 5-0.
    "Wachezaji wengi wamemaliza mikataba yao, wapo baadhi huenda wakaongezewa kama Chuji, lakini wengine watatemwa akiwamo Shamte ambaye hakuna ubishi hatarudi Jangwani msimu ujao," alisema mtoa habari.
    Alisema wachezaji Nurdin Bakari, Hamis Kiiza, Kenneth Asamoah bado wana mkataba wa mwaka mmoja, wakati Yaw Berko na Davis Mwape mikataba yao itamalizika Novemba mwaka huu.
    "Uongozi umeshaanza kuzungumza na Berko kuangalia uwezekano wa kuongeza mkataba wake, lakini Mwape hatacheza Yanga msimu ujao mara baada ya mkataba wake kumalizika," alisema mpashaji huyo habari.
    Jumamosi wiki hii Kamati ya Utendaji itakutana, na moja ya mambo watakayozungumza ni ushiriki wa Ligi Kuu, changamoto zilizokuwepo na kujadili wachezaji watakaochwa na wanaostahili kubaki.
    "Kikubwa kinachoangaliwa ni nidhamu wa wachezaji ndani na nje ya uwanja pamoja na kiwango, na pia kuna wachezaji wengine watahama kwenda timu nyingine haya yote yataangaliwa."
    Alisema ajenda nyingine kwenye kikao hicho ni kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu wa wanachama pamoja na vuguvugu la mgogoro lililopo ndani ya klabu hiyo.
    Mwenyekiti wa Yanga Llody Nchunga alisema masuala yote yanayohusu usajili wa wachezaji watawekwa wazi wiki ijayo mara baada ya kikao chao cha Kamati ya Utendaji.
    Aidha, kuhusu wachezaji wanaodai, Nchunga alisema ni wale waliongezewa mikataba ambao ni Nurdin Bakari na Nadir Haroub.
    "Wachezaji wanaodai fedha za usajili ni wachache tena waliongezewa mikataba kipindi cha uongozi uliopita na hata hivyo fedha hizo wanatakiwa walipwe msimu ujao kwa kuwa ndiyo watakaoanza kuutumikia," alisema Nchunga na kuwataja wachezaji hao kuwa ni Nurdin na Nadir.
    "Nawashangaa wazee wetu wanavyosema wachezaji wanadai Sh127 milioni. Hivi hawa wazee ni wahasibu? Wamepata wapi hesabu hizi, napenda kuwaambia kuwa hatudaiwi kiasi hicho," alisema.
    Kuhusu shinikizo la kutakiwa kujiuzulu, Nchunga alisema hawezi kufanya hivyo kwa shinikizo la watu wachache wakati Yanga ni timu ya wanachama.
    "Mimi nilichaguliwa na wananchana wa Yanga, wao ndiyo wanaweza kunitaka nijiuzulu tena kupitia Mkutano Mkuu wa Klabu. Tunaendeshwa na katiba na siyo kelele za vikundi vya watu. Hatima yangu itaamuliwa na Wanayanga, siyo kikundi.
    "Kamati ya Utendaji itapanga tarehe ya Mkutano Mkuu, mimi nafuata katiba na wala sing'ang'anii madaraka Yanga. Wale wote wanaotaka mimi na uongozi wangu tujiuzulu, basi waje kwenye mkutano mkuu," alisema bosi huyo.
    Alisema utamaduni wa kuondoa madarakani uongozi kwa njia za mkato umepitwa na wakati. "Mambo ya kupinduana yamepitwa na wakati, dhambi hii ya kupinduana haitaishia kwa Nchunga peke yake itawatafuta wengine. Ifike mahali tubadilike tufanye kazi kwa kufuata katiba na siyo mazoea."
    Aliongeza: "Wanaona sifai wafuate taratibu na watoe sababu za msingi siyo kwa vile tumepokwa pointi tatu ndiypo wanishinikize nijiuzulu hayo ni makosa ya soka.
    Naomba itoshe kusema hivi...wale wote wanaodhani nitajiuzulu nafasi yangu, ni wazi wamepitwa na wakati. Sijiuzulu kwa sababu ya kikundi cha watu wachache, wanachama ndiyo wataamua."
    Kuhusu madai ya kocha wa Yanga Kostadin Papic, Nchunga alisema: "Papic tunamuandalia malipo yake ambayo ni mishahara ya miezi miwili na muda wowote atalipwa.
    Alikiri uongozi wake kutokuwa na ushirikiano na Papic kwa sababu kocha mwenyewe amekuwa akionyesha dharau mbele ya uongozi kwa kushindwa kuheshimu maagizo anayopewa.
    "Sikiliza nikuambie, Papic hatuwezi kuwa naye tena tunamuandalia chake aondoke, kwanza hata wachezaji hawamtaki. Tulishawahi kumuonya kuhusu kutoa mambo ya ndani ya klabu kwenye vyombo vya habari lakini hakuwahi kutekeleza agizo hilo.
    "Mechi ya Toto kule Mwanza alichangia kwa kiasi kikubwa tukapoteza mchezo. Kwanza alikataa kwenda na timu, baadaye akataka atumiwe tiketi aende Mwanza akatumiwa kufika tu wachezaji wakakosa raha.
    Hata hivyo Nchunga hakutaka kuweka wazi mbadala wa Papic kwa madai kuwa Kamati ya Utendaji ndiyo itakayoamua hatima yake. Hata hivyo kuna taarifa klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kupitia vielelezo vya makocha kutoka Romania na Scotland.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NCHUNGA AUNGURUMA, TISA HATARINI KUTEMWA YANGA, MROMANIA KUMRITHI PAPIC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top