![]() |
| Kaburu kushoto, akiwa mtambo wa mabao wa Msimbazi, Emmanuel Okwi |
DERRICK Walullya, beki wa kimataifa wa
Uganda na mshambuliaji Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati rasmi
hawatasajiliwa Simbs SC msimu ujao, wakati huo huo wachezaji wanne wazawa
mikataba yao inaisha Juni, mwaka huu.
Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY
asubuhi hii, Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amewataja
wachezaji ambao mikataba yao inaisha ni kipa Ally Mustafa Mtinge ‘Barthez’,
mabeki Juma Said Nyosso, Juma Hamisi Jabu na kiungo Uhuru Suleiman Mwambungu
‘Robinho’.
“Hawa wa kigeni kwa kweli hatutawaongezea
mikataba, ila hawa wa nyumbani naona wengi wao wakiwa fiti wanacheza vizuri,
hasa mashindano ya nyumbani. Tutazungumza nao, tukiafikiana tutawaongezea
mikataba,”alisema Kaburu.
Kaburu alisema mazungumzo ya mikataba mipya
yatafanyika baada ya Simba kumaliza kabisa msimu wa mashindano- ila kama
watafuzu kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, zoezi hilo litafanyika
Juni.
Akimzungumzia mshambuliaji Abdallah Juma wa
Ruvu Shooting, ambaye inadaiwa amesajiliwa na klabu hiyo, Kaburu alisema;
“Bado”.
Akaongeza: “Huyu mchezaji amependekezwa na
wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji tumsajili, na yeye ameonyesha nia haswa ya
kuchezea Simba, tulichofanya tumezungumza naye tu,”alisema Kaburu, ambaye kesho
asubuhi anakwea ‘pipa’ kuelekea Sudan, kuungana na timu yake, ambayo Jumapili
itacheza na Al Ahly Shandy katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 Bora,
Kombe la Shirikisho la Afrika.
Katika mchezo huo, Simba inahitaji sare tu
ili kusonga mbele, kwani mchezo wa kwanza ilishinda mabao 3-0 Dar es
Salaam.



.png)
0 comments:
Post a Comment